Habari Kali
Loading...

FUTARI YAZUA BALAA! APEWA KIPIGO CHA MBWA MWIZI BAADA YA KUIBA KITI


Dustan Shekidele, Morogoro LA haula! Mwanamke aliyefahamika kwa jina moja la Asha, mkazi wa Mtaa wa Area Six, Kata ya Kichangani mkoani  hapa ambaye alikuwa kwenye swaumu ya Mfungo wa Ramadhani, amejikuta akilazimika kutengua swaumu na kumpa kichapo mwanaume aliyeiba futari na kiti chake cha plastiki alichokuwa amekalia nje ya nyumba akipika futari hiyo.
Akihojiwa baada ya kuminyiwa kichapo.
TUKIO KAMILI
Tukio hilo la aina yake, lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo wakati paparazi wetu anawasili kwenye eneo la tukio, alikuta kasheshe bin tafrani ikiendelea. Mbali na mwanamke huyo, wananchi wenye ghadhabu nao walikuwa wakimshikisha adabu mwanaume huyo huku wakidai ni mwizi.

MAELEZO YA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo, awali mwanamke huyo alikuwa nje ya nyumba yake akipika futari huku akiwa amekalia kiti hicho.


Akiomba kuachiwa baada ya kupewa kichapo kikali.
“Ghafla si akapata udhuru uliomlazimu aingie ndani. Akaacha futari ikitokota jikoni. Amefanya yake kule ndani, akakumbuka ameacha futari jikoni, akatoka.“Kufika! Kwanza akaona futari imepungua. Sasa ile anataka kukaa, kiti nacho hakipo. Akashangaa.”
ATAFUTA KITI, AMWONA NACHO MTU
Chanzo kiliendelea kudai kuwa, mwanamke huyo alianza kukisaka kiti chake sehemu mbalimbali nyumbani hapo lakini bila mafanikio. Alipotupa macho mbali na nyumbani, akamwona nacho huyu mwanaume amekibeba akitambaa zake.

“Ndipo mama bila kujali swaumu, akaingia ndani. Akachukua kirungu na sime na kumfukuza mpaka akamkamata na kuanzia kumwangushia kipondo huku jamaa akikitupa kile kiti kichakani kwa lengo la kupoteza ushahidi,” kilisema chanzo hicho.
WANANCHI WAINGILIA KATI
Baadhi ya wananchi wanaoaminika kuwa na hasira kali nao waliamua ‘kununua’ kesi hiyo ambapo na wao walichukua silaha mbalimbali, yakiwemo mawe na kuanza kumbonda mwanaume huyo mpaka damu chapachapa.

Anayedaiwa kuibiwa futari akimpiga kwa hasira.
BODABODA NUSURA WAMTOE UHAI, WAMVUNJA MGUU
Baadhi ya madereva wa bodaboda walipomwona mwanaume huyo anazidi kuchakaa uso kwa kipigo, badala ya kumwokoa, waliingilia kati na kutaka kumchoma moto lakini wasamaria wema walipinga kitendo hicho na kumuokoa kwa kumkimbizia kwenye Kituo cha Polisi cha Nanenane kilicho jirani na eneo la tukio.

Hata hivyo, wakati akikimbizwa polisi, bodaboda hao waliamua kumgonga na pikipiki kwa makusudi na mmoja wao alifanikiwa kumvunja mguu.
MAMA MWENYE FUTARI
Alichonifanyia siyo haki kabisa, kama alikuwa na njaa, angeniambia, ningempakulia futari akala kuliko kuniibia.

ACHAKAZWA SURA NA MKE MWENZIYE


Na Stephano Mango, Ruvuma
“Dunia imeharibika na binadamu hawana upendo wamegeuka kuwa na tabia kama za wanyama kila kukicha…” hiyo ni kauli yake Rehema Gwaya (41) mkazi wa Barabara ya Sokoine, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Rehema Gwaya akiwa na majeraha usoni baada ya kumwagiwa mafuta ya moto.
Rehema ambaye ni mjasiriamali mdogo anayejishughulisha na kuuza juisi, alipatwa na mkasa wa kumwagiwa mafuta ya moto ya kupikia ambayo yalikuwa yanatumika kwa ajili ya kuchomea maandazi.
Inadaiwa aliyefanya unyama huo ni mke wa  shemeji yake baada ya kutokea sintofahamu ya usafi wa mazingira ya nyumbani kwao, kama anavyojieleza:
“Tukio limetokea mwishoni mwa Mei nikalazwa mwanzoni mwa Juni hadi sasa Julai ambapo Daima Said (13) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Luseti ninayeishi naye aligombana na mke wa shemeji yangu, Zefania Chimgege, chanzo kikiwa ni suala la usafi wa mazingira kwani mama huyo alipaswa kwenda kusafisha choo akakataa kukawa na mzozo mkubwa.
“Mzozo huo ulitokea mimi nikiwa sipo, nilikuwa kwenye biashara zangu, niliporudi nyumbani nilimfuata mama Chimgege ili anipe maelezo, ghafla akanivamia na kuanza kunishambulia kwa maneno makali yaliyoambatana na matusi.

Akimnyonyesha mwanaye.
“Wakati huo mume wake alikuwa anachoma maandazi kwa ajili ya biashara yake, wakati naendelea kutafakari kauli chafu alizozitoa dhidi yangu, nilishitukia nikimwagiwa mafuta ya moto usoni, papo hapo nilianguka chini jambo  lililompa nafasi mama huyo kunikalia na kuanza kunichuna ngozi iliyobabuka.
“Nilipoteza fahamu na kujikuta nipo Hospitali ya Mkoa Songea, nimelazwa wodi ya wanawake nikiwa na majeruhi usoni na kwenye matiti, hivyo naendelea kupata matibabu.
“Nawaomba Watanzania wenye mapenzi mema kunisaidia kwani kwa sasa siwezi kufanya shughuli yoyote kutokana na kuuguza majeraha ya moto ambayo yana maumivu makali na hapa nilipo nina mtoto mdogo wa miezi tisa ambaye ananyonya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea, Dk. Benedikto Ngaiza amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo ambapo alisema anaendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,  ACP Mihayo Mikhela amekiri kutokea kwa tukio hilo na amethibitisha kuwa mtuhumiwa anashikiliwa wakati upelelezi unaendelea.

MAHABUSU ADAIWA KUFIA KITUO CHA POLISI!


Na Shani Ramadhani MSIBA! Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Juma Abdallah Juma (51), mkazi wa Bunju ‘B’ jijini  Dar anadaiwa kufia kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar huku ndugu wakiibuka na madai kuwa, alipigwa na polisi wa kituo alichowekwa mahabusu, Uwazi lilifuatilia.
Marehemu Juma Abdallah Juma enzi za uhai wake.
Akizungumza na gazeti hili, dada wa marehemu Juma, Mwanaidi Abdallah alisema, awali, marehemu na ndugu zake wawili, Muhisan (42) na Baraka (30) walikamatwa Juni 16, mwaka huu na askari wa vituo vya polisi vya Wazo, Boko na Tegeta kwa madai wanahusika na wizi wa magari matatu.
Ndugu huyo alisema, askari hao waliyataja magari hayo kuwa ni Toyota Prado (thamani ya Sh. milioni 30), Mistubishi (Sh. milioni 30) na BMW (Sh. milioni 65). 
Iliendelea kudaiwa kuwa, askari hao waliwachukua na kuwapeleka vituo tofauti ambapo, Muhisan alipelekwa  Kituo cha Tegeta, marehemu Juma, Wazo na Baraka alisukumizwa Boko.
“Baada ya kusikia hivyo, tulikwenda Tegeta, tulimkuta Muhisan, akatuambia Juma yupo Kituo cha Polisi Wazo lakini hali yake si nzuri (hakufafanua kivipi). Lakini baadaye wote walihamishiwa Kituo cha Kawe. Tulipofika huko pia tukazuiwa kumuona, polisi wakasema ndugu yetu ni jambazi.
“Tulihangaika sana. Baada ya wiki moja tukamuona tena kwa kuomba kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wazo. Kusema kweli hali yake ilikuwa inasikitisha. Alikuja kutusalimia akiwa anatambaa, amevimba uso, mikono, miguu yote na mmoja ulikuwa umepasuka.
“Tuliomba apelekwe hospitali  kufanyiwa uchunguzi tujue anasumbuliwa na nini, tukaambiwa tutoe shilingi 15,000  nauli ya Bajaj.
“Siku ya pili tulipokwenda tukakuta amefungwa bandeji kwenye miguu, wakasema tumnunulie dawa ya kupunguza maumivu, tukafanya hivyo.“Mke wa Muhisan alidamka kupeleka chai kwa mumewe, kufika akaambiwa ndugu zenu wote leo wamepelekwa Mahakama ya Kinondoni.
“Tulipopata taarifa hizo... tulijipanga na wadhamini tukaenda mahakamani. Kufika tukakuta ndiyo wameitwa na wakati huo Juma amebebwa na Muhisan na Baraka hawezi kutembea sawasawa. Walisomewa mashitaka  yao kuwa waliiba magari kwenye Yadi ya Mazrui iliyopo Kijitonyama (Dar) wakiwa wametumia silaha aina ya bastola.
“Washitakiwa wakaandikiwa kwenda Gereza la Segerea lakini wakaambiwa gari limejaa, ikabidi wapelekwe Kituo cha Polisi Oysterbay kukaa kwa muda.
“Jumanne ya wiki iliyopita, tukapeleka chakula asubuhi, Juma hakuweza kula. Tulipokwenda baadaye, Muhisan akasema hali ya Juma ni mbaya. Tukafanya mpango wa  gari la magereza akatibiwe lakini kabla gari halijafika, polisi walikwenda kumchukua kwa kumbeba kwenye machela, wakamuweka kwenye gari, kabla hawajaondoka, Juma alikata roho.
“Sisi tulitoka pale kwenda Hospitali ya Mwananyamala na wao walielekea huko. Walipofika wakaufikisha mwili moja kwa moja mochwari,” alisema Mwanaidi kwa huzuni.
Ili kujua ukweli wa mambo yota hayo, Uwazi lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camillius Wambura ambaye alikiri kuwa na taarifa za kifo cha Juma, lakini akasema:
“Juma aliletwa hapa baada ya kukosa nafasi kwenye  gari alilokuwa anatakiwa kupanda kwenda Segerea. Habari za kupigwa au kutokupigwa zitatafsiriwa baada ya uchunguzi kufanyika kwa sababu mpaka sasa mwili wake bado upo mochwari kwa uchunguzi (kesho).
“Mtuhumiwa alifariki dunia baada ya kuugua akiwa kituo cha polisi kabla ya kupelekwa hospitali kupata matibabu ya ugonjwa wake.”

UKATILI WA KUTISHA! MTOTO MIAKA 5 ATEKWA DAR, ABAKWA HADI KUFA


Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
NIkweli dunia imekwisha! Ni vigumu kuamini mtoto mdogo ambaye anahitaji uangalizi na ulinzi kutoka kwa jamii anageuzwa mwanamke na kuingiliwa kwa nguvu hadi mauti. Huu ni unyama na ukatili wa hali ya juu.

Mtoto Ester Banzi enzi za uhai wake.
Tukio hilo la kutisha lilitokea katikati ya wiki iliyopita, Tabata Msimbazi jijini Dar ambapo mtoto Ester Banzi ,5, (pichani) alikutwa na mauti baada ya kuingiliwa kimwili na mwanaume ambaye inadaiwa alimteka kwanza.
Akizungumza na Gazeti la Uwazi kwenye msiba huo, mama mdogo wa marehemu Ester aliyejitambulisha kwa jina la Watende Hamis huku akitokwa machozi mfululizo, alisema:

“Siku ya tukio, ilikuwa saa 5:30 asubuhi tukiwa nyumbani, dada (mama wa marehemu aitwaye Rebeka) alikuwa ameinjika sufuria ya ugali jikoni kwa ajili ya chakula cha mchana.
“Akamtuma Ester dukani akanunue unga. Alimpa shilingi 1,200. Si mara ya kwanza Ester kutumwa dukani kwa vile ni jirani tu.

“Tulimsubiri Ester arudi na unga lakini alichukua muda mrefu. Ikabidi tumfuate dukani, hatukumuona. Tuliwauliza watoto wenzake ambao anapenda kucheza nao, wakasema walimuona amebeba mfuko cha Rambo huku akiongozana na baba mmoja.

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu likiwa tayari kwa ajili ya kuagwa.
“Basi, tuliendelea kumtafuta bila mafanikio. Ikabidi tutoe taarifa kwa baba yake ambaye akaingiwa na wasiwasi, akaenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Tabata Shule.“Ndani ya masaa matatu baba yake akatupigia simu kwamba mwili wa Ester umeokotwa huku ukionekana alibakwa na kuharibiwa vibaya.”
Naye kijana anayeuza duka ambalo marehemu alitumwa kununua unga, bila kutaja jina lake alikiri Ester kufika dukani hapo na kupimiwa unga kisha akaondoka.
Baadhi ya wananchi majirani na maeneo hayo waliohojiwa na waandishi wetu kuhusiana na tukio hilo walisema kwamba wao walimuona mtoto huyo akifuatana na mwanamume mmoja, lakini hawakumtilia mashaka kutokana kwamba walifikiri ni ndugu yao.
Mtu mmoja ambaye mwili wa marehemu ulikutwa jirani na nyumba yake, naye alizungumzia tukio hilo:
“Sisi tulisikia sauti ya mtoto akiomba msaada. Tulipata hofu ikabidi tukaangalie eneo lile ndipo tulipouona mwili wa mtoto huyo. Tulipomchunguza tukagundua alibakwa kwani nguo yake ya ndani ilikuwa pembeni.

“Inaonekana huyo mtu hakuchukua muda mrefu kufanya kitendo hicho. Tulimpigia simu Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata Shule, Afande Kobelo akaja na timu yake. Hili tukio nahisi lina ushirikina ndani yake.”
Mmoja wa askari aliyefika katika eneo la tukio ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa vile siyo msemaji mkuu wa jeshi hilo alisema mwili wa mtoto huyo ulionekana kuingiliwa kimwili, marehemu alivunjwa shingo na kutobolewa upande wa kushoto kichwani.Marehemu Ester alizikwa wiki iliyopita mkoani Morogoro. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu. Amina.

MAITI YAKOHOA, YAFUMBUA MACHO

1Maajabu ya Bagamoyo! Katika hali ya kushtua, familia yenye makazi yake, Magomeni, Bagamoyo mkoani Pwani, imejikuta kwenye mauzauza baada ya ndugu yao kufariki dunia huku akidaiwa kukohoa, kufumbua macho na kuonesha dalili za kuwa hai, pamoja na kwamba daktari alithibitisha kifo.
WAOMBOLEZAJI WATIMUA
Katika tukio hilo lililosababisha waombolezaji kutimua mbio lililojiri Juni 28, mwaka huu, binti wa familia hiyo, Tunu Shabani (36), alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kutokana na kuumwa kichwa ghafla.
MUME ASIMULIA
Akizungumza na Amani lililofunga safari kutoka Dar hadi Bagamoyo, mume wa Tunu, Iddi Ramadhani alisema mkewe alianza kupata maumivu ya sikio baadaye kichwani ambapo alimhamishia kwa wazazi wake maeneo hayohayo ya Magomeni kwa kuwa ni karibu na hospitali.
Iddi alisimulia kuwa Juni 27, mkewe huyo alipelekwa kwenye hospitali hiyo, akatundikiwa dripu lakini hali ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kuwekewa mashine ya kupumulia kabla ya kuaga dunia alfajiri ya Juni 28.
“Baada ya daktari kuthibitisha kifo cha mke wangu, ndugu tulikutana, tukaandaa mazishi kwa kuchimba kaburi na shughuli ya kuandaa maiti kwa ajili ya mazishi tuliyopanga yafanyike saa 6:00 siku ya pili yake yaani Juni 29.
“Wakati wa kuosha maiti mara tukasikia sauti kasha ikafumbua macho, miguu yake ikajinyoosha na mwili ukawa na joto.
“Ilibidi tusitishe kumzika kwanza na kujaribu kumtafuta daktari,” alisema Idd.
Aliongeza kuwa, hali ya marehemu iliendelea kuwatatiza kwa kuwa wataalam walishindwa kufanya chochote hadi Juni 29, walishangazwa zaidi kuona maiti ikiwa inatoka jasho jingi huku joto likiendelea kuwa vilevile.
SHEHE ANENA
Akizungumza na waandishi wetu, shehe aliyekuwa akisimamia kuandaa maiti, Mtawa Adam (pichani) alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu za mazishi za Dini ya Kiislam, marehemu ambaye ni mwanamke huoshwa na wanawake wenzake, kanuni ambayo mwili wa Tunu nao uliipitia.
Shehe Adam alisema kuwa, kama kawaida alimpima marehemu na kumshonea sanda huku akisubiria wanawake hao wamalize kumuosha na kumuandaa ili yeye aingie kwa ajili ya kumnyosha viungo, lakini kabla hawajamaliza, alishtushwa kuwaona wakitoka mbio na kudai maiti imefumbua macho na kunyoosha mguu.
“Niliingia ndani na kumuona marehemu ambapo wakati huo alikuwa amefumba macho, nilipomgusa alionekana wa moto kama alikuwa hai, nikamtazama nyayo zake zilionekana ni nyeupe tofauti na za marehemu ambazo huwa za njano.
“Nilimrekebisha mguu wake aliounyoosha, lakini nikashangaa ukirudi tena kama ulivyokuwa awali na hata mapigo yake ya moyo yalikuwa yakipiga mara moja baada ya dakika hata mbili,” alisema shehe huyo na kuongeza kuwa aliwashauri wanafamilia wamuondoe Tunu kwenye kitanda cha maiti na kughairi maziko huku daktari mwingine akiitwa kumpima lakini naye alisema alifariki dunia.
UMATI WAJAA
Waandishi wetu, walishuhudia umati wa waombolezaji wakiwa wamezunguka eneo hilo ili kushuhudia kilichoendelea.
MAMA APANDISHA MASHETANI
Katika hali isiyo ya kawaida, mama mmoja alipandisha mashetani na kudai Tunu hajafa.
WAGANGA WANNE
Kwa mujibu wa ndugu mmoja wa familia hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, waliwaita waganga wa nne wa kienyeji ambapo mmoja alifika na kudai Tunu alichukuliwa msukule lakini alishindwa kumfanya awe hai.
Aidha, waganga waliobakia licha ya kufanya ndumba zao, Tunu hakuweza kuamka kama walivyodai awali.
Baba mzazi wa marehemu, Adam Hassan akizungumza na waandishi wetu alisema Tunu hakuonesha dalili za kuwa hai hivyo taratibu za mazishi zilifanyika kesho yake (Juni 30) na kuzikwa katika Makaburi ya Kiwangwa, Bagamoyo.

MWALIMU SEKONDARI AKAMATWA NA ‘UNGA’

Na Makongoro Oging’
Mwalimu wa shule moja ya sekondari mkoani Singida (jina la shule linahifadhiwa), Charles Andrew (46) amekamatwa na Kikosi Kazi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini (task force) katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akidawa kuwa na mzigo wa ‘unga’ pipi 101 ya aina ya heroin yenye zaidi ya shilingi milioni mia moja.

Mwalimu wa shule moja ya sekondari mkoani Singida (jina la shule linahifadhiwa), Charles Andrew (46) anayedaiwa kukamatwa na unga.
Taarifa kutoka vyanzo vyetu makini ndani ya kikosi hicho zinasema kwamba mwalimu huyo alikamatwa Juni 25, mwaka huu, saa kumi alfajiri akijianda kusafiri kwenda nchini Ghana kupitia Nairobi.
Habari zaidi zinadai kwamba mwalimu huyo alipokamatwa alikutwa na pipi 40 akiwa amezificha sehemu za siri na baadaye alitoa pipi 61 ambazo alimeza tumboni.


Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa alipoulizwa ofisini kwake na mwandishi wetu juzi alikiri kukamatwa kwa mtu huyo na kiasi hicho cha madawa.
“Tulipata taarifa kutoka kwa raia mwema ndipo tukaweka mtego na tukafanikiwa kumkamata mtu huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu wa shule ya sekondari huko mkoani Singida, hata hivyo tutamfikisha mahakamani wakati wowote upelelezi ukikamilika,” alisema Kamanda Nzowa.
Kamanda Nzowa amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaotoa juu ya wauza na watumiaji wa unga na waendelee kushirikiana na polisi ili kukomesha kabisa biashara hiyo haramu.

INASIKITISHA SANA..!! DENTI KIDATO CHA KWANZA AFIA BWAWANI!

Na Kulwa Mwaibale MSIBA! Mohamed Juma (14) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari ya Toangoma wilayani Temeke, Dar amefia bwawani wakati akiogelea.
Tukio hilo lililoacha majonzi kwa ndugu, jamaa, marafiki na wanafunzi wenzake, lilijiri Juni 26, mwaka huu, majira ya alasiri.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari ya Toangoma wilayani Temeke, Dar, Mohamed Juma (14) amefia bwawani wakati akiogelea.
Akizungumza na Uwazi kwa masikitiko makubwa ya kumpoteza mwanaye, baba mzazi, Juma Shaha alisema familia yake imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mtoto wao wa kiume.
“Nashindwa nianzie wapi kuzungumza maana tumepata pigo kubwa sana kuondokewa na mwanangu wa kwanza katika uzao wetu wa watoto watatu wa kiume, inauma sana kwa kweli,” alisema Juma.
Juma alisema, majira ya saa 4 asubuhi ya siku ya tukio, Mohamed aliaga  kwenda twisheni na baadaye saa 8 kuelekea 9 alasiri alikwenda kwa rafiki zake Kilakala, Kongowe.
“Jambo la kushangaza, hadi inafika saa 2 usiku, Mohamed hakuonekana nyumbani ndipo tulianza kumtafuta,” alisema mzazi huyo.
Baba Mohamed alisema alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kongowe ambapo walimweleza aendelee kumtafuta.
Aliongeza kuwa, baada ya hapo alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tuangoma ambaye aliungana naye kumtafuta bila mafanikio.
Juma alisema kuwa, licha ya kutoa taarifa Polisi Kongowe, alishauriwa kuripoti pia Kituo Kikuu cha Polisi Mbagala-Maturubai.
Alisema, wakati akirejea nyumbani kutoka kituoni, mkewe, Rahma Juma alimpigia simu na kumfahamisha kwamba rafiki zake Mohamed  walipeleka nguo za marehemu nyumbani.
Aliendelea kusimulia kuwa, walipowahoji watoto hao, Gabriel na Musa walisema wakati wakijiandaa kuogelea kwenye bwawa hilo lililopo Toangoma, walimuona nyoka mkubwa ndipo walichukua nguo na kukimbia wakimuacha Mohamed.
Mzee huyo alisema walipokwenda Toangoma alikokutana na Mkuu wa Sekondari ya Toangoma, Nchimbi na vijana kadhaa wakaenda kwenye bwawa hilo.
Walipofika, vijana wanaoweza kuogelea walijitosa kwenye bwawa kumtafuta Mohamed ambapo walifanikiwa kumuibua akiwa amenasa kwenye matope huku ameshafariki dunia.
Mzazi huyo alisema kwamba, katika jambo la kushangaza, Mohamed hakunywa maji kama inavyokuwa kwa watu wanaokufa vifo vya ajali ya maji.
“Baada ya polisi kufika walinihoji nikawaeleza kisa cha mwanangu kufariki dunia ndipo wakauchukua mwili kwenye gari na kuupeleka nyumbani kwangu, tukafanya taratibu za mazishi na kumzika katika Makaburi ya Kimicha yaliyopo hukuhuku Kongowe,” alisema Juma kwa huzuni

INASIKITISHA: FAMILIA YATUPIWA YATUPIWA VYOMBO NJE!


Shani Ramadhani na Mayasa Mariwata
USIOMBE yakukute! Beatrice Nyato au mama Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, anapika, anapakua na kulala nje ya nyumba yake baada ya kutupiwa vyombo nje na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Anwar ambaye ni mkurugenzi wa kampuni moja ya usafirishaji ya jijini Dar.

Beatrice Nyato au mama Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, anayepika, anapakua na kulala nje ya nyumba yake.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, mama Prisca alisema kasheshe hiyo ilimkumba yeye na wapangaji wake.
Alisema awali alikwenda katika ofisi za mkurugenzi huyo kwa lengo la kuuza nyumba yake ili amlipie mume wa binti yake deni la benki ambapo yeye ndiye alimdhamini kupitia nyumba hiyo.

Vitu vya familia hiyo vikiwa nje ya nyumba.
“Nilisikia ile kampuni huwa inanunua nyumba. Nilipofika, tukaongea na mkurugenzi, akanipa mtu nije naye ili aione. Nyumba yangu ni kubwa, ina vyumba kumi na sehemu ambayo unaweza kupaki magari madogo hata kumi.
“Yule mtu alipoiona akaenda kumwambia bosi wake, kesho yake naye akaja kuiona.  Kuhusu bei, nilimwambia Sh. milioni 600, yeye akasema parefu. Nikashuka hadi Sh. milioni 500, akasema atanipa Sh. milioni 400 lakini baadaye akasema atanipa milioni 320 ili milioni 80 iwe kwa ajili ya kuhamisha wapangaji, bili ya maji na umeme. Nikakubali,” alisema mwanamke huyo.
Mama Prisca alisema, waliandikishiana kwenye karatasi kwa makubaliano ya kuanza kulipa pesa anazodaiwa benki, zinazobaki kumlipa kupitia cheki.
Bosi huyo, kwa mujibu wa mama Prisca, aliahidi kuanza kulipa shilingi milioni 150 kwa ajili ya benki (jina lipo) na nyingine angemalizia baadaye.

Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, akipika nje ya nyumba yake.
“Siku kadhaa mbele alinipigia simu akasema atanipa afisa niende naye benki kwa ajili ya kufuatilia hati kwa kuwa yeye atakuwa safirini. Nikaambiwa mimi na mkwe wangu tuandike barua iende benki.
“Baada ya wiki mbili nikapigiwa simu na benki kuwa deni la Sh. milioni 50 limeshalipwa.
“Kulikuwa na deni la pili, benki nyingine, mkurugenzi akasema hawezi kulipa bila mimi kutoa hati ya nyumba, nikampa, akalipa benki Sh. milioni 70,” alisema mama huyo.
Mama Prisca alikuwa akiendelea kudai Sh. milioni 80 ambayo walikubaliana ilipwe kupitia cheki lakini alipokwenda kwa ajili ya kujaza fomu ili aingiziwe fedha yake hiyo alishangaa kuambiwa malipo yameishia pale na hakuna zaidi ikiwa na maana kwamba, nyumba ilinunuliwa kwa Sh. milioni 270  tu!
 “Nilimfuata tena, akaja juu, akasema nataka nini tena? Huku akinitolea maneno makali kuwa yeye ni mgonjwa nampigia kelele, akasema niondoke asije akaniitia polisi.


“Hivi karibuni, sijui siku gani ile! Saa 5:00 asubuhi, walikuja watu waliojitambulisha kuwa wanatoka kampuni ya udalali wakiwa wameongozana na mabaunsa kama 10 na askari 15, wakadai wametumwa na aliyenunua nyumba kuibomoa.
“Mimi sikuwepo, hata wapangaji walikuwa kwenye shughuli zao, lakini kaka yangu alikuwepo. Aliwazuia kwa kuwataka waende kwanza serikali za mtaa lakini wakagoma.
“Kaka alinipigia simu na kunipa taarifa, nikachanganyikiwa, nikakumbuka nina fedha ndani, nikamwambia atoe mfuko wenye fedha, akasema haupo ila mimi nifanye ninavyoweza niwahi.
“Nilipofika, niliwakuta mabaunsa na polisi wenye silaha wameizingira nyumba. Nikazuiliwa kuingia kwa kuambiwa kuna kazi inaendelea.
“Majirani zangu wakaja kunivuta pembeni na kuniambia mama Prisca utazimia utupe kazi ya kukupepea au utakufa kwa presha. Nikakaa pembeni wakinipepea, baadaye wakaniondoa kabisa eneo lile.
“Wakati naondoka, nikampigia simu wakili wangu, akaniambia suala langu linatakiwa lifikishwe mahakamani. Mpaka leo ni siku ya 10, tunalala hapa nje, ndani kuna walinzi wenye silaha, wanaingia kwa shifti. Geti limefungwa na mnyororo.
 “Wapangaji nao baada ya kukuta vyombo vyao vipo nje wakapaniki, wakasema watanipiga vinginevyo niwape fedha ya kulala gesti na fedha ya chakula. Jumanne iliyopita wakanipeleka Kituo cha Polisi Chang’ombe, nikalala siku moja, siku ya pili nikapelekwa Kituo cha Polisi Kilwa Road nikalala, kesho yake nikatolewa kwa dhamana.
Baada ya kutoka kwa mama Prisca, waandishi wetu walikwenda kwenye ofisi za mkurugenzi huyo zilizopo Kurasini ambapo walinzi waliwazuia kuingia ndani wakidai hairuhusiwi.
Jumamosi iliyopita, waandishi wetu walikwenda tena lakini mtu mmoja aliyekataa kujitambulisba alisema ishu ya mwanamke huyo ipo polisi (bila kutaja kituo) hivyo mkurugenzi huyo hawezi kusema lolote na hakukuwa na kiongozi yeyote ofisini hapo.

MTOTO WA WAZIRI ATUHUMIWA KWA KUUA!

Deogratius Mongela na Chande Abdallah INASIKITISHA! Mmiliki wa Shule ya Msingi na Awali (International) ya Mount Zion iliyopo Bahari Beach, Dar, Annah Mizighi Mwambili, 47, (pichani) ameuawa na mwili wake kutupwa ndani ya shule yake baada ya kupotea kwa zaidi ya miezi sita huku mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tatu Ntimizi, Said Ntimizi akidaiwa kuwa mmoja kati ya watuhumiwa wa mauaji hayo.
Mmiliki wa Shule ya Msingi na Awali (International) ya Mount Zion iliyopo Bahari Beach, Dar, Annah Mizighi Mwambili enzi wa uhai wake.
Duru za awali za upelelezi wa polisi, zinamtaja Said kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na marehemu bila kufafanua alihusikaje na mauaji hayo ya kinyama yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana, siku na tarehe isiyojulikana na mwili wake kutupwa kwenye shimo la maji taka ndani ya eneo la shule aliyokuwa akiimiliki.
Aidha, nyuma ya taarifa hiyo ya mauaji, deni la shilingi milioni mia tisa (900,000,000) ambalo mwanamke huyo alikuwa akimdai mmoja kati ya watuhumiwa hao ambao majina yao yote bado hayajafahamika likitajwa kuwa ndiyo chanzo cha Annah kutolewa uhai.

ALIANZA KWA KUTOWEKA
Wakisimulia kwa uchungu namna Annah alivyotoweka nyumbani kwake, ndugu wa marehemu walisema, awali Desemba 26, mwaka jana kwenye Sikukuu ya Boxing Day, kuna wageni walifika nyumbani kwake, Boko, Dar, wakazungumza na baadaye wakaondoka naye na hakurudi tena.

Mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tatu Ntimizi, Said Ntimizi anayedaiwa kuwa mmoja kati ya watuhumiwa wa mauaji hayo.
NDUGU WAPATA WASIWASI, WATOA TAARIFA POLISI
Ndugu hao walisema kuwa siku za kwanza hawakupata wasiwasi kwa vile ilikuwa kawaida ya marehemu kuwa mtu wa safari kutokana na biashara zake na kuongeza kuwa walianza kupata wasiwasi baada ya siku nne kupita huku kukiwa hakuna mawasiliano kati yao na marehemu, jambo lililowalazimu kuripoti Kituo cha Polisi cha Wazo Hill ambao walianza uchunguzi.

WAUMINI WAFUNGA NA KUSALI
Wakati wote huo, waumini wa kanisa alilokuwa akisali marehemu Annah la Winners Chapel lililopo Ukonga jijini Dar waliamua kufanya maombi ya kusali na kufunga kwa ajili ya kumuomba Mungu awaoneshe  mpendwa wao alipo.

MAITI YAPATIKANA SHULENI KWAKE MIEZI 6 BAADAYE
Kwa masikitiko makubwa, ndugu hao walisema, Juni 22, mwaka huu, ikiwa ni miezi sita na siku na chache tangu kupotea kwa ndugu yao, walipata taarifa iliyowashtua na kuwaumiza, kwamba mwili wa mpendwa wao umepatikana ukiwa umeharibika vibaya ndani ya shimo la maji machafu katika shule yake.

Ndugu, jamaaa na marafiki wakiwa katika misa ya mazishi.
HABARI ZA CHINICHINI
Habari za chinichini ambazo si rasmi zilizonyakwa na Gazeti la Uwazi, zinaeleza kuwa baada ya marehemu huyo kuchukuliwa nyumbani kwake, inadaiwa watuhumiwa walikwenda naye mpaka kwenye nyumba ya mganga mmoja maarufu wa kienyeji (jina kapuni) ambako walimuua kisha kuuchukua mwili wake na kuutupa shimoni.

POLISI WANASA TUKIO
Kama Waswahili wasemavyo, damu nzito kuliko maji ndivyo ilivyokuwa kwa Annah ambaye damu yake iliendelea kuwasumbua wahusika kiasi cha unyama wao kuwafikia polisi kupitia njia za kijasusi na hivyo kufanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa.
“Polisi walipopata taarifa za mauaji hayo, waliamua kufuatilia, wakabaini mmoja kati ya watuhumiwa hao yuko Arusha. Wakamuwekea mtego na kufanikiwa kumnasa, wakamleta jijini Dar ambapo aliwataja aliodai kushirikiana nao,” chanzo kutoka vyombo vya usalama kililiambia Uwazi.

MWALIMU MKUU AZUNGUMZA
Akizungumza na Uwazi, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dony Maige alisema shule yake ilikuwa imefungwa wakati marehemu ambaye ni mmiliki na mkurugenzi akiwa hajulikani alipo.
“Januari mwaka huu, tarehe za mwanzoni tulifungua shule kama kawaida baada ya likizo ya Desemba ambapo wanafunzi waliendelea na masomo. Lakini bajeti ilikuwa ngumu kutokana na mkurugenzi ambaye ndiye mtoaji wa fedha za matumizi ya shule na malipo ya wafanyakazi, kutoonekana.
“Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wazazi kulazimika kuchangia huduma nyingine muhimu japokuwa walikuwa wamemaliza ada za watoto wao.

MWALIMU AWATOA MACHOZI WAOMBOLEZAJI
“Juni 21, mwaka huu tukiwa tumefunga shule na kutarajia kufungua tena kwa ajili ya muhula mpya wa masomo, ndipo nilipopokea simu kutoka vyombo vya usalama na kunitaka kusitisha zoezi la kufungua shule kwa kuwa kutakuwa na oparesheni maalumu katika eneo la shule. Nikaambiwa niwaondoe wafanyakazi wote isipokuwa mimi peke yangu.
“Nilishangaa, baada ya kufika shuleni na kuwaona polisi wakiwa eneo la tukio. Nilishtuka kutokana na maswali waliyokuwa wakiniuliza. Lakini jambo lililonishtua zaidi ni kuuona mwili wa marehemu Annah ukitolewa ndani ya shimo la maji machafu lililopo ndani ya shule ambayo kwa miezi yote sita wanafunzi na hata sisi walimu tulikuwa tukipita bila kujua.
“Kwa kweli sijawahi kukutana na kipindi kigumu kama hiki katika maisha yangu. Ni jambo la ajabu sana. Nimejiuliza maswali mengi na kukosa majibu,” alisema mwalimu huyo huku waombolezaji wakishindwa kuzuia machozi yaliyokuwa yakiwatiririka.

MWILI WAAGWA BILA KUFUNULIWA
Wakati wa kuuaga mwili huo, Jumamosi iliyopita nyumbani kwa marehemu, waombolezaji walitoa heshima zao za mwisho kwa masikitiko mbele ya jeneza la marehemu bila kufunuliwa kutokana na mabaki ya mwili huo kuharibika vibaya.
Mwili wa marehemu Annah ulipumzishwa katika Makaburi ya Kwakondo, Ununio jijini Dar. Hakika bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina. Marehemu ameacha watoto watatu, Steven, Irene na Emerly Mwambili.

POLISI KINONDONI WALIVYOSEMA
Uwazi lilimpigia simu Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Emanuel Mlei na kumuuliza yafuatayo.
Uwazi:  “Kuna madai kwamba, mtoto wa aliyewahi kuwa waziri kwenye serikali ya awamu ya tatu, Tatu Ntimizi, Said Ntimizi mnamshikilia kwa mauaji ya mwanamke aliyekuwa mmiliki wa shule, Annah Mwambili, ni kweli?”
Kamanda: “Kuhusu hilo siwezi kulisema kwa sasa. Ila kesho (jana) nenda pale kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova ataliongelea yeye.”
Uwazi bado liko kazini kuchimba tukio hili la kinyama na kwamba litaendelea kuwaletea mapya kadiri yanavyopatikana.

IMAMU: NIMEMWAGIWA TINDIKALI KUTETEA MALI ZA MSIKITI


Na Musa Mateja UNYAMA wa kutisha! Bwana mmoja ambaye ni imamu, aliyefahamika kwa jina la Mustafa Omar Mustafa, mkazi wa Ghana, Kata ya Nyamanoro jijini Mwanza, amefanyiwa unyama wa hali ya juu kwa kumwagiwa tindikili na watu wanaosadikiwa kuwa ni waumini wenzake, kisa kulinda mali za msikiti wao uliopo katika mtaa huo wa Ghana. Uwazi linakupa habari kamili.
Mustafa Omar Mustafa, anayedaiwa kumwagiwa tindikali.
ILIKUAJE?
Akizungumza na mwandishi wetu kwa masikitiko Mustafa alisema kuwa, tukio hilo la kinyama alifanyiwa majira ya saa mbili kasorobo usiku, Jumapili ya Agosti 31, mwaka jana akiwa nyumbani kwake Ghana.

“Nilikuwa katika hali ya furaha na familia yangu, sikuhisi kabisa hatari ambayo ilikuwa inakuja kutokea katika maisha yangu. Tukiwa hatuna hili wala lile, tulishitukia kundi la watu likivamia nyumba yangu ndipo waliponitendea unyama huu na kutoweka,” alisema.
AKIMBIZWA HOSPITALI YA MKOA SEKOU-TOURE
 “Baada ya unyama huo familia yangu na jamaa wa karibu kwa haraka walinikimbiza katika kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo ambapo nilipata kibali cha matibabu (PF3) na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-toure, ambapo nilipokelewa na kuingizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.“Katika chumba hicho nilikaa kwa muda wa siku sita nikahamishiwa katika chumba cha wodi za kawaida.”

Mustafa akionyesha jeraha alilolipata mkononi.
MATIBABU YASHINDIKANA AHAMISHIWA CCBRT
“Baada ya hali yangu kuzidi kuwa mbaya, madaktari wa hospitali hiyo walinishauri kufanya utaratibu wa kwenda kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya CCBRT Dar ambayo inasifika kwa kutoa huduma nzuri ya matibabu ya macho.

“Kama unavyoona sehemu kubwa niliyoathirika na tindikali ni usoni, kifuani na mgongoni! Mwanzoni kabisa macho yote hayakuwa yanaona ndipo nilipohamia CCBRT, ambapo angalau nimeweza kupata matibabu, namshukuru Mungu sasa jicho moja la kulia linaweza kuona kwa mbali.
KISA CHA KUMWAGIWA TINDIKALI
 “Kabla ya tukio hilo katika msikiti wetu kulikuwa na mgogoro kati ya waumini na viongozi wa msikiti.
Hatukuwa tunawataka ambapo baada ya mvutano wa muda mrefu uliosababisha kufikishwa  mahakamani baadhi ya watu, uchaguzi wa viongozi wengine ulifanyika chini ya uangalizi maalumu wa mahakama, baada ya kupatikana viongozi wapya nilipendekezwa kuwa imamu na nikawa naongoza sala za asubuhi.

Jeraha la kifuani.
“Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, nilianza kujihusisha na shughuli mbalimbali za msikiti ikiwemo kufanya usafi wa mazingira  na kutunza baadhi ya rasilimali jambo ambalo lilionekana kutolifurahisha kundi la baadhi ya watu ambao hawakuwa wanaupenda huo uongozi mpya, ambapo kwa kile walichokiita kunikomesha ndipo walipoamua kunimwagia tindikali.
MSAADA
“Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi niliyonayo, nawaomba Watanzania watakaoguswa na matatizo yangu kunisaidia ili niweze kupata huduma ya matibabu zaidi kwani hali yangu kiuchumi kwa sasa ni mbaya sana.

“Nawashukuru sana wote ambao wamenisaidia mpaka angalau nimekuwa katika hali hii, japo hali yangu bado haijawa vizuri sana hasa kimaisha, maana nimeshatumia fedha zangu zote kwa ajili ya matibabu na leo hii nafikia hatua ya kuomba kwa kuwa familia inanitegemea na haina namna tena, mtaji wangu wote umeishia katika matibabu.
“Kabla ya kufanyiwa unyama huu nilikuwa wakala wa mitandao ya simu na sasa changamoto yangu kubwa ni hali ya hewa ya jijini Dar es Salaam kuwa ya joto sana, hivyo napata maumivu sana kwenye majeraha yangu.
Jeraha la mgongoni.
MACHO
 “Hivi sasa matibabu ya macho bado yanaendelea ingawa nimeambiwa nirudi tena mwezi ujao (Juni) ambapo nimepewa uhamisho kwenda katika Hospitali ya Ocean Road kwa ajili ya kushughulikia tatizo la ngozi ambayo nayo imeharibika vibaya.

“Nilikwenda katika hospitali hiyo nikaambiwa kumuona daktari tu, natakiwa kutoa shilingi elfu hamsini, kiasi ambacho kwa sasa ni kikubwa sana kwangu maana nakosa hata shilingi mia mfukoni.“Ninayoyasema hapa ni rahisi kwa asiye jua hali yangu kuona kama natania ila ukweli ni kwamba hata fedha ya kwenda hospitali kumuona huyo daktari sina.
“Nawaomba Watanzania wanisaidie ili niweze kumuona daktari kisha nipate nauli ya kurudi Mwanza kukaa na familia yangu japokuwa siwezi kuihudumia. Changamoto ni kwamba baada ya mwezi natakiwa kurudi Dar kwa matibabu ya macho na ngozi.
“Nampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo kwa kuwa nami bega kwa bega tangu nipate tatizo hili na hakika yeye ni mtu mwenye upendo wa dhati, pia nawashukuru wote ambao wanaendelea kunijulia hali,” alisema Mustafa huku akilengwalengwa na machozi.
 Aliyeguswa na habari hii awasiliane naye kwa namba 0752 362 221, kutoa ni moyo.

A-Z MTOTO ALIVYONYONGWA MOROGORO

Na Dustan Shekidele, Morogoro SIKU tatu baada ya mazishi ya mtoto Edyline Barnabas Mafwere (9), aliyedaiwa kuuawa kwa kunyongwa na mtoto wa baba yake mkubwa, simulizi kamili imepatikana baada ya ndugu jamaa na majirani wa marehemu kuzungumza na gazeti hili.
Marehemu Edyline Barnabas Mafwere enzi za uhai wake.
Judith, msichana anayedaiwa kufanya mauaji hayo ambayo yamegeuka kuwa gumzo mjini hapa, anadaiwa alijaribu kumuua msichana huyo mara ya kwanza Mei 10, mwaka huu, lakini akashindwa baada ya jirani mmoja kumuwahi na kumkuta akiwa amemkaba shingo.
Mwenyekiti mstaafu wa serikali ya mtaa huo, Hasda Msuya alisema akiwa nyumbani kwake, siku hiyo alisikia sauti ya mtoto akilia kwa muda mrefu, alipokwenda katika nyumba hiyo alimkuta Judith akimpiga marehemu huku akiwa amemkaba shingo, lakini akamkemea na kuondoka zake.
Mama mzazi wa Edyline Barnabas Mafwere akilia kwa uchungu.
“Jana (Mei 20, 2015) majira ya saa 12 jioni nilisikia kilio kwa mbali, wakati najiandaa kwenda, Judith akaja kwangu na kunieleza Edyline ameanguka na kutoka damu mdomoni, nilipokwenda nilikuta kweli hali hiyo nikampigia simu mama yake, alipofika tumekuta tayari mtoto amekufa, lakini tukaamua kumpeleka hospitali na madaktari wakathibitisha alishafariki muda mrefu,” alisema mama Msuya.
Mmoja wa wanafamilia hiyo aliyesafiri na wazazi wa mtuhumiwa wa mauaji hayo, alisema haelewi kwa nini baba na mama walishindwa kuhudhuria mazishini licha ya kuwa walishafika Morogoro.
Jeneza lililobeba mwili wa Edyline Barnabas Mafwere likiandaliwa kwa ajili ya mazishi.
“Sisi ni wakazi wa Ukerewe, wazazi wa Judith wamefika jana, wamefikia gesti moja ipo Kichangani wakiwa miongoni mwa watu tisa, lakini sijui sababu ya wao kushindwa kufika mazishini,” alisema mwanafamilia huyo huku akiomba hifadhi ya jina lake.
Baba mzazi wa marehemu, Barnabas Mafwere alisema siku ya tukio alikuwa kazini hivyo hana maelezo marefu, lakini akasema alimchukua mtoto huyo wa kaka yake ili aishi naye kama mwanaye kabla ya kupokea taarifa za kitendo chake cha kumnyonga mwanaye.
Akiongoza lbada ya mazishi Padri John Greyson wa Kanisa la Kolla la Mwili na Damu ya Yesu, aliwaliza watu baada ya kusema marehemu alikuwa miongoni mwa watoto waliokuwa wapokee Ekaristi Takatifu mwishoni mwa mwaka huu.
Wanafunzi wakiuaga mwili wa mpendwa wao Edyline Barnabas Mafwere.
Naye mwakilishi wa Shule ya Kata ya Kolla Hill aliyokuwa akisoma Judith, Mwalimu Neema Lupena alisema ni jambo la kusikitisha kuwa mtuhumiwa wa mauaji ni mwanafunzi wao wa kidato cha kwanza, lakini akasema alipokelewa shuleni hapo licha ya nafasi kujaa kutokana na heshima ya baba yake mdogo.

MAAJABU WATOTO KUFIA KWA GWAJIMA

Stori: Waandishi Wetu “KWA kweli sisi kwetu kama kanisa ni maajabu na mshtuko. Inapotokea ajali kama hii bila kutarajia lazima kutokee mshtuko. Hakuna anayependa kutokea kwa hali hii, tumuombe Mungu. Najua mengi yatasemwa lakini ukweli ni kumuachia Mungu tu,” ndivyo alivyoanza kusema Askofu Yekonia Byabaza ambaye ni Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Marehemu Sarah enzi za uhai wake.
Askofu Byabaza aliyasema hayo alipozungumza na Gazeti la Uwazi kufuatia vifo vya watoto wawili ndugu wa damu moja, Sarah (10) na Goodluck David Oturo (4) waliokufa kwa kunaswa na umeme wakiwa kwenye ibada katika kanisa hilo, Kawe jijini Dar wiki moja iliyopita.
Askofu huyo alizungumza na Uwazi kwenye ibada maalum ya kuaga miili ya marehemu hao iliyofanyika nyumbani kwa wazazi, Mbezi Juu jijini Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita.
Aliendelea kusema: “Ninachokijua ni kwamba hali hiyo imetokea kwa wote baada ya Goodluck ambaye ni mdogo alipoona dada yake amenaswa na umeme alimfuata na kumgusa huku akilia na kusema; dada… dada…ndipo na yeye akanaswa lakini siyo kwamba kuna jambo. Mungu alipanga kuwa vifo vyao vitatokana na njia hiyo.”
Marehemu Goodluck enzi za uhai wake.
MASWALI YA WANAFUNZI
Katika msiba huo uliowaacha midomo wazi waombolezaji, wanafunzi waliokuwa wakisoma na Sarah walikuwa na maswali kwa muda mrefu:

“Kwa nini iwe familia hiyo tu? Kwa nini iwe Sarah na mdogo wake tu? Mbona kulikuwa na watoto wengi! Halafu tunasikia waya uliomnasa Sarah haukuwa umechubuka, sasa kwa nini anaswe?”
Wanafunzi hao muda mwingi walikuwa wakitokwa machozi kupindukia huku wengine wakiishiwa nguvu.
Mmoja wa wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Samuel alisema kwamba, Sarah alikuwa mpole na alikuwa akipatana na kila mmoja, hakuwa mgomvi na alikuwa ana uwezo mkubwa darasani.

Mama wa marehemu hao akilia kwa simanzi kubwa wakati wa kuaga miili hiyo.
KITAALAM
Mtu mmoja msibani hapo ambaye alijitambulisha kuwa ni fundi umeme, alisema kuwa, kwa umeme wa majumbani, mtu akivaa viatu hata kama atakanyaga waya wenye umeme si rahisi kunaswa na kufa.
“Napata shida sana kama kweli Sarah alikanyaga waya wenye umeme. Mbona alivaa viatu tena viatu vyenyewe havikuwa na chuma, kwa nini anaswe? Haya kwangu ni maajabu hasa ninapoambiwa hata huo waya wenyewe haukuwa umechubuka,” alisema fundi huyo.

MAJIRANI, WAALIMU WAZIMIA
Ili kuonesha kuwa, vifo vya watoto hao viligusa wengi, baadhi ya majirani sambamba na walimu wa marehemu Sarah, jumla yao ikipata tisa, walianguka na kupoteza fahamu wakati wakipita kwenye majeneza kuiaga miili hiyo.


Baba wa marehemu hao(katikati) akiaga miili ya wapendwa wake.
MSEMAJI WA FAMILIA
Kutokana na hofu na mkanganyiko wa vifo hivyo kutanda, gazeti hili lilizungumza na ndugu wa karibu wa marehemu hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini na kumuuliza juu ya maoni ya familia hiyo ambapo alikuwa na haya ya kusema:

“Kwa kweli kwangu haya ni maajabu! Mimi si msemaji mkuu wa familia lakini ninachokijua ni kwamba, marehemu kabla ya vifo vyao  walishatuhangaisha sana kwa kuumwa, hasa Goodluck. Na ajabu ni kwamba, kuumwa huko, tulipowapeleka hospitali hawakupata nafuu lakini tulipowapeleka kwa waganga wa kienyeji walipona.
“Kifupi ni kwamba, ukisimuliwa historia ya maisha yao kwa ujumla ilitafsiri vifo. Inatuuma sana! Ajabu ya magonjwa yao, walikuwa wakipelekwa kwa waganga wa kienyeji wanapata nafuu.“Baba yao amehangaika nao mpaka basi hali iliyomfanya mama yao kuamua kuwapeleka katika maombi kwa Askofu Gwajima.”
Wanafunzi wakilia kwa uchungu.
Msemaji huyo: “Nakumbuka Goodluck akiwa na umri wa miaka miwili, siku moja tukiwa ndani ya nyumba iliibuka harufu ya dawa za kienyeji, ghafla yeye alianza kunyooka huku akipoteza fahamu. Alipelekwa hospitali ikashindikana, akapelekwa kwa waganga wa miti shamba akapata nafuu.”
MWAKA MMOJA BAADAYE
“Baada ya mwaka moja alianza kuumwa tena, akawa anatembea huku akizunguka huku na kule bila kusema na mtu. Alionekana kama yupo kwenye ulimwengu wa pekee. Aliweza kupona kwa mganga.

Mmoja wa waombolezaji akiwa amezimia.
“Safari ya tatu akawa anatembelea makalio huku Sarah naye akianza kuumwa tumbo na kuwa mpole sana. Tuliamua kuwapeleka hospitali mbalimbali lakini hawakupona, tulipowapeleka kwa mganga wa miti shamba wakapona.
“Ndipo tulipogundua kuwa kuna mchezo mchafu unafanyika na hapo ndipo mama yao akawa anakwenda nao katika maombi. Nafikiri mengi zaidi mkamuulize baba yao.”

WAZAZI WASIMULIA
Baba mzazi wa marehemu hao, David Oturo yeye kwa upande wake alikiri kuumwa kwa watoto hao magonjwa ya ajabu ambapo alipokuwa akiwapeleka hospitali hawakupona bali walipata nafuu walipopewa dawa za kienyeji.“Na mimi nimepatwa na mshtuko kuhusiana na vifo vya watoto wangu.

Waombolezaji wakiwa na nyuso za majonzi.
Nimehangaika nao kwa muda mrefu na nilijua wameshapona, ndiyo maana nilimruhusu mama yao kwenda nao kwenye maombi. Sikutegemea kama mauti yangewakuta wote kwa siku moja kule kanisani. Lakini yote namuachia Mungu,” alisema kwa masikitiko mzazi huyo.
Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa marehemu hao alisema:
“Vifo vya watoto wangu siku hiyo kama niliviona tangu nyumbani. Ajabu ni kwamba, moyo wangu siku hiyo ulikuwa na ganzi kwenda kanisani. Lakini nikajipa nguvu tukaenda, kumbe ningeusikiliza moyo nikaacha kwenda, wanangu wasingekufa.

“Lengo la kuwapeleka kwa Askofu Gwajima ni kuombewa ili magonjwa ya ajabuajabu yawatoke, wawe salama nikijua hata kukwepesha vifo vyao maana kusema ule ukweli mimi na mume wangu tulihangaika nao sana, nikajua kwa Gwajima ndiyo nimefika kumbe bado!
Majeneza yaliyobeba miili hiyo yakiombewa kwa ajili ya mazishi.
MIILI YASAFIRISHWA
Miili ya watoto hao ilisafirishwa Ijumaa iliyopita kwenda Musoma mkoani Mara kwa mazishi yaliyofanyika Jumamosi. Oturo kwa sasa amebaki na mtoto mmoja wa kiume, mkubwa kwa wote.

Uwazi linatoa pole kwa familia ya Oturo kwa msiba mkubwa uliowapata na Mungu awape uvumilivu. Bwana ametoa Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe! Amina.Imeandaliwa
Older Posts
© Copyright ZEE LA UDAKU | Designed By Code Nirvana
Back To Top