Habari Kali
Loading...

SLIM AANGUA KILIO GARI LIKIENDA KWA MTALAKA

MUIGIZAJI mahiri wa filamu, Slim Mbegu ‘Slim’ hivi karibuni aliangua kilio akiwa Mahakama ya Mwanzo Magomeni baada ya kushuhudia gari alilopewa zawadi yeye na mkewe aliyetengana naye, Asia Morgana likivutwa kwa Break Down kusogezwa eneo hilo.
Muigizaji mahiri wa filamu, Slim Mbegu ‘Slim’.
Wawili hao walikuwa na shauri mahakamani hapo wakigombea gari hilo kila mmoja akidai ni mali yake halali, lakini hatimaye mwanamke alishindwa na hivyo Slim kuamriwa kulipeleka kortini ili liweze kukabidhiwa kwa wenyewe, lakini akashindwa kwa kushindwa kulifanyia matengenezo madogomadogo ya kulifanya litembee.
Gazeti hili liliongea na Asia aliyemshukuru Mungu kwa kuweza kupata gari lake alilodai kusumbuliwa kwa muda mrefu na aliyekuwa mumewe, wakati Slim alisema hana la kusema zaidi ya kumuachia Mungu kila kitu.

Wema Sepetu: Hata mimi Ningekuwa Aunty Ezekiel Ningegombana na Wewe

Oscar ndauka
LICHA ya kupatana, habari ya mjini kwa sasa ni ugomvi mkali, wenye visa  vya kushangaza kati ya mastaa wawili wa sinema za Bongo, Wema Sepetu na Aunt Ezekiel.Hii ‘kapo’ siku za karibuni, ilikuwa nzuri kwa maana ya urafiki wao mkubwa.Urafiki wa Wema na Aunt ulianza pale Wema alipoutengua urafiki wake na staa mwingine wa fani hiyo, Kajala Masanja.

Kuna visa lukuki kuhusu chanzo cha ugomvi wa Wema na Kajala, lakini ‘kuchukuliana’ bwana ndiyo kulitajwa sana!
Ikumbukwe kuwa, Kajala naye alirithi kijiti cha urafiki kwa Wema kutoka kwa msanii wa filamu na Mbongo Fleva, Snura Mushi.

TUREJEE KWA AUNT
Katika urafiki ambao ulionekana ungedumu zaidi ni kati ya Wema na Aunt kwa vile, Aunt alionekana kama mkomavu wa mambo ya ukaribu kuliko wengine, Snura na Kajala.Sasa siku za hivi karibuni, Magazeti Pendwa ya Global Publishers (ambayo huwa ya kwanza kufichua mambo ya siri ya mastaa), yaliandika kuhusu uhasama ulioibuka kati ya wawili hao chanzo kikiwa ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.

Mpenzi wa sasa wa Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari’ aliandaa shoo aliyoiita Zari All White Party iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar.

UGOMVI ULIANZA KWENYE PROMO
Inajulikana kwamba, mtu anapoandaa shoo, kikubwa ni kuipigia ‘debe’ kwa maana ya kwamba, watu wajue kuna shoo kubwa ili waweze kuhudhuria kwa wingi na ndiyo mafanikio ya mwenye kuandaa! Wakati shoo hiyo ikipigiwa debe na vyombo mbalimbali vya habari sambamba na wadhamini, Aunt aliandika ujumbe wa kuisifia, kwamba itakuwa ya nguvu na si ya kukosa, akaitupia kwenye mtandao wake wa Instagram.

AUNT MNAFIKI?
Habari zilimfikia Wema kwamba, Aunt ametupia kwenye ukurasa wake akiisifia shoo ya Zari All White. Hapo ndipo pakawa pabaya kwa Wema akitafsiri kwamba, kitendo hicho kwake ni kibaya kwa sababu Zari yupo na Diamond ambaye yeye alikuwa mpenzi wake zamani, akammwaga! Tena hapa ieleweke sawa, Wema ndiye aliyemmwaga Diamond.

Kumbe Wema anaishi na kinyongo cha Zari kwa sababu amemchukua ‘wa zamani’ wake, Diamond. Kwa hiyo ana bifu! Akitokea mtu akampa 5 Zari, kwa Wema mtu huyo anakuwa adui kama ilivyokuwa kwa Aunt Ezekiel ambaye ameonekana ni mnafiki! Anachekaje na Zari wakati Zari na yeye ni maadui?! (eti).

KWA NINI AUNT ALIFANYA VILE LAKINI?
Aunt alikuwa na kila sababu ya kuifagilia shoo ile kwa sababu moja kubwa sana! Ameshamwanika mpenzi wake wa sasa kwamba anaitwa Moses Iyobo! Huyu dogo ni dansa kwenye kundi la Diamond. Kwa hiyo shoo za Zari ilitegemea sana madansa wa Diamond.

Hivyo, Aunt alitumia nafasi hiyo kuwataka watu wafike kwa wingi, ukumbi ujae kutokana na kiingilio na waonesha shoo, akiwemo Iyobo walipwe vizuri, ili maisha yake na Aunt ambaye kwa sasa ni mjamzito, yaendelee. Sasa Wema alitakaje? Aunt aseme; ‘msiende shoo ya Zari, itakuwa mbaya sana’! Halafu ‘mzee’ (Iyobo) aende kula za uso? Ni akili kweli?

HUU NI UTOTO!
Mimi nauona huu ni utoto uliopitiliza! Katika hilo la Wema kumwona Aunt ni msaliti au mnafiki, hata mimi kama ningekuwa Aunt ningegombana na Wema na wala moyoni nisingeona nimepoteza chochote!

AUNT NA IYOBO
Naamini Aunt na Iyobo bado wapo sana kimaisha kuliko Aunt na Wema. Mbaya zaidi ukizingatia Wema mwenyewe kila rafiki anayempata anampoteza kwa uadui! Maana yake nini sasa!

Mimi namshauri (Wema) akae chini na kutafakari kwa mapana mwenyewe, na si kwa kushauriwa na akina Petit Man au Martin Kadinda, ajiulize ni kwa nini yeye! Na si kujiuliza ni kwa nini marafiki zake wengi humaliza nao vibaya!
Anaweza kuamini ana nuksi kumbe si nuksi bali ni maisha ya ubinafsi! Cha kwake anataka akiendeshe yeye na cha wenzake pia anataka akiendeshe yeye, hayo si maisha Wema bwana! Chenji!

Source:Global Publishers

Mtitu Amjibu Steve Nyerere "Ukifa Mimi Napata Faida Gani ? Kanumba Amekufa Akiwa na Bifu na wewe Chanzo ni Hayo Maneno yako"

Mtitu ameandika haya mara baada ya kuona alichokiandika Steve Nyerere

"Da ! Naomba ndugu zangu
mnisamehe kwa kuandika hili humu instagram ...maana lilitakiwa liongelewe nje ya hapa ...
kiukweli steve NIMESHTUKA SANA baada ya kuona post yako tena umenihuzunisha sana kwa kunitaja kwa jina katika ugomvi wako na dude nimejaribu kukupigia cm sana aupokei cm zangu aukupokea na
Umesema.

kuwa natamani ufe...hv tujiulize kwa nini nitamani ufe ndugu yangu ?? So ukifa mimi napata faida gani ? Kwani mimi nna ugomvi gani na wewe?? kwanza tunafanya vitu tofauti na mimi producer na msambazaji wewe mchekeshaji kwa nini nigombane na wewe ?? kwani nn steve utaki kujifunza mdogo wangu maneno haya haya yamesababisha Kanumba amekufa huku akiwa awaongei na Ray wakati walikuwa marafiki kwa zaidi ya miaka kumi na Kanumba amekufa huku ukiwa na bifu kubwa sana na wewe nae wewe hadi anakufa mlikuwa amuongei chanzo ni haya haya maneno yako ...

Kuwa na amani steve wewe ni mhehe kama mimi kwetu kumoja miongoni na mwa watu ambao sitawasahau katika maisha yangu wewe ni mmoja wa wao, umenisaidia vitu vingi sana nakushukulu mangere ..na pamoja uliapa ukiwa na matatizo nisije mimi ntakuja tu labda unifukuze wewe kama unahisi mimi mbaya wako umekosea mimi sina ubaya na wewe kabisa na sioni sehemu pa kutugombanisha maana atuna tunapokutana" Mtitu

JOHARI NILIKUWA MAMA NTILIE!

KABLA hajaanza ‘kuuza sura’ kwenye runinga, Blandina William Wilbert Chagula ‘Johari’ alikuwa akijihusisha na kazi ya upishi na uuzaji wa chakula biashara ambayo aliifanya jijini Dar kabla hajajiunga na Kundi la Sanaa la Kaole baada ya kuhitimu mafunzo ya Hotel Management.
Staa katika tasnia ya filamu Bongo, Blandina William Wilbert Chagula ‘Johari’.
Johari alianza kupika na kuuza chakula kwenye catering ya shangazi yake huku akihangaika kutafuta njia ya kutimiza ndoto yake ya uigizaji aliyokuwa nayo tangu akiwa kijijini kwao Bugoyi mkoani Shinyanga.Johari anasema aliamua kusomea masomo ya upishi kwa kushinikizwa na ndugu zake walioamini kuwa ana uwezo mkubwa wa kupika chakula kizuri na kitamu japo moyoni mwake hakuwa na ‘hobi’ hiyo.
“Kabla ya kutimiza ndoto yangu hii ya uigizaji, nilikuwa napika na kuuza chakula, si unajua katika maisha kabla hujatimiza ndoto na malengo yako ni lazima uhangaike kwa kupitia vikwazo na vizingiti vingi?
“Hivyo mimi nilijikuta nikiangukia kwenye u-hotelia japo sikuwa interested kabisa, lakini kwa sasa namshukuru Mungu kwa kuwa nimetimiza ndoto yangu,” alisema Johari katika mahojiano maalum na mwandishi wetu hivi karibuni.

STEVE NYERERE ANADAIWA KULA FEDHA ZA KUJENGEA KABURI LA KUAMBIANA!


Waandishi wetu TAKRIBAN mwaka mmoja tangu mwigizaji Adam Kuambiana aiage dunia, kaburi lake limeibua skendo ya wasanii kudaiwa ‘kuchikichia’ fedha za kulijengea, Amani lina full stori.
Mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ akiwa kwenye kaburi la marehemu Kuambiana.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini, kaburi la nguli huyo wa sinema lilipokuwa linatimiza mwaka mmoja, ilidaiwa lilitoka fungu la shilingi milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ili zijengee kaburi hilo lakini zikazuiwa kwanza kwenye mifuko ya mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’.

“Wiki moja kabla ya shughuli ya misa ya kutimiza mwaka mmoja kifo cha marehemu, Nyerere (Steve) alipewa alipewa shilingi milioni moja, akakaa kimya hadi kaburi likajengwa na mke wa marehemu Julieth Lite (Diwani wa Kunduchi) kwa kutumia fedha zake,” kilisema chanzo hicho.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.
UBUYU WAZIDI KUMWAGWA
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, siku moja kabla kumbukumbu iliyofanyika Jumapili iliyopita (Jumamosi), mjane wa marehemu alipokea shilingi laki saba kutoka kwa mtu aliyejisajili kwa jina la Albert Msando akimwambia ni mchango wa Makonda wa kujengea Kaburi.Baadaye iliingia shilingi laki tatu kwenye namba nyingine ya simu ambayo ilielezwa kuwa ni mchango wa kujenga kaburi uliotoka kwa mwigizaji Jacob Steven ‘JB’.

STEVE NYERERE AJINADI
Wakati maandalizi ya misa yakiendelea, Jumamosi jioni, Steve Nyerere na baadhi ya wasanii walitupia picha kwenye mtandao wa kijamii huku wakisindikiza na ujumbe uliojinasibu kuwa wanamshukuru Mungu kuashiria wamefanikisha kujengea kaburi hilo kitu ambacho kilikanushwa baadaye na mwigizaji Kulwa Kikumba ‘Dude.’
“Jamani hakuna msanii aliyehusika kujengea kaburi zaidi ya mke wa marehemu, Julieth Lite,” aliandika mitandaoni Dude ambaye ni mdogo wa Julieth.

Mwigizaji Kulwa Kikumba ‘Dude.’
MJANE AFUNGUKA
Amani lilimvutia waya mjane wa marehemu Kuambiana, Julieth ambaye naye alisisitiza kuwa kaburi hilo alilijenga kwa fedha zake mwenyewe.“Nilijenga mwenyewe lakini wakati tunakaribia kufanya misa (Jumamosi) nakumbuka ilikuwa kama saa tano na nusu usiku,  ghafla nilipokea shilingi laki saba kutoka kwa Msando nikaambiwa ni za Makonda na baadaye nikapokea laki tatu nikiaambiwa ni za JB,” alisema Julieth.

NYERERE ANASEMAJE?
Amani lilipomtafuta Steve Nyerere na kuulizwa kama ni kweli alipewa shilingi milioni moja na Makonda kisha akakaa kimya na kama zile laki saba zilizokabidhiwa na Msando zinahusiana na zile alizopewa na Makonda, alijibu:

“Ninavyojua mimi hizo fedha hajatoa Makonda, tumetoa sisi wasanii kama huamini ongea na JB huyu hapa (akampa simu).
“Tulitoa sisi wasanii, kama ulikuwepo siku ile pale makaburini ungeona alichoongea mke wa Kuambiana. Ni sisi kaka ndiyo tumetoa. Wewe mpigie mke wa marehemu halafu muulize alichosema siku ile makaburini halafu nipigie tena,” alimalizia JB na kukata simu.

Alipopigiwa Makonda ili aweze kudadavua kiundani juu ya fedha alizotoa na nani aliyempa alijibu:
“Nipo katika kikao unaweza kunitumia meseji?”
Licha ya kutumiwa meseji, hadi tunakwenda mitamboni, hakuwa ametoa jibu lolote.

WASANII WANASWA KWA UFUSKA

Brighton Masalu
SHABAASH! ‘Makinda’ wawili wanao penyapenya katika sanaa ya maigizo runingani wa Kundi la Sanaa la Jakaya Theatre Arts Group, Sefu Ngao ‘Stefano’ na Vanessa Msofe wamenaswa wakifanya uchafu kwa kuoneshana mahaba mazito huku wakiwa ‘bwii’, Ijumaa Wikienda linakupa ishu nzima.
Wasanii hao wakiwa katika mahaba mazito baada kulewa.
Tukio la uchafu huo unaotia kichefuchefu cha ‘mimba changa’, lilinaswa na ‘kiona mbali’ cha gazeti hili namba moja kwa skendo na ufuska wa wasanii, waigizaji na mastaa mwishoni mwa wiki iliyopita maeneo ya Sinza-Legho jijini Dar na kuzua mshangao mkubwa.
Wasanii hao wakiendelea na starehe zao....
Kitendo cha wasanii hao kufanya uchafu huo kisa ulevi, kilikatishwa na mmoja wa wahudumu wa baa hiyo.
“Jamani nilipeni hela yangu na muondoke hapa,” alisikika mhudumu huyo aliyekerwa na vitendo vichafu vya wasanii hao.

BONGO MOVIE WAMLIZA MAMA LORAA!


Na Imelda Mtema
Baadhi ya mastaa wa tasnia ya sinema za Kibongo wanaounda Klabu ya Bongo Movie, wamemliza laivu mlezi wao ambaye amekuwa akiwasapoti kwa hali na mali, Catherine Ambakisye ‘Mama Loraa’ baada ya kumuangushia bonge la pati la kushtukiza (suprise) ambalo hakulitarajia.

Catherine Ambakisye ‘Mama Loraa’.
Wahusika hao walimfanyia Mama Loraa pati hiyo hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Baloko uliopo maeneo ya Vijana-Kinondoni jijini Dar ikiwa imeandaliwa na mastaa wa kike wa Bongo Movie.
Baadhi ya mastaa hao walioshuhudiwa na gazeti hili ni pamoja na Jennifer Kyaka ‘Odama’, Halima Yahya ‘Davina’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Salma Salmin ‘Sandra’, Herith Chumila na wengine, ikiwa ni kuthamini mchango wake mkubwa aliuofanya katika kukuza tasnia ya filamu Bongo.
Akizungumza huku akitokwa machozi, Mama Loraa alifunguka: “Sikuwa na mpango wowote wa kufanya kitu chochote lakini nimeshangazwa na maandalizi haya yaliyonitoa machozi ya furaha maana sikutarajia.”
Katika sherehe hiyo, walimwalika mumewe Loraa ambaye hakujua kuna shughuli ambapo alikabidhiwa zawadi ya ua kwa ajili ya siku yake hiyo.Wasanii hao walimpa Mama Loraa zawadi mbalimbali vikiwemo viatu, magauni na vitu vingine kisha watu wakaanza kunywa na kula hadi wakasaza.

Barua Nzito: Wastara Omba Radhi‭, ‬Badilika‭!‬

KWAKO mwanamke unayejua kuuvaa vyema uhusika katika sinema za Kibongo, Wastara Juma. Za siku nyingi? Uko poa mama!?

Ukitaka kujua afya yangu mimi ni mzima wa afya, naendelea na mishemishe zangu za kila siku kuhakikisha mkono unakwenda kinywani. Nimekukumbuka hapa leo maana ni kitambo kidogo hatujaonana. Nikaona ni vizuri kukuandikia barua.

Dhumuni la barua hii ni kwanza kutaka kukukumbusha juu ya heshima niliyokuwa nakupa. Nilikuwa nakuheshimu kama mama wa watoto wawili, mtu mzima mwenye busara za kutosha.

Kwa levo ya heshima niliyokuwa nakupa, sikuwahi kuwa na shaka kwamba labda kuna siku unaweza ukabadilika. Niliamini kadiri siku zilivyozidi kusonga ndivyo busara zaidi zingeendelea kujaa katika kichwa chako.

Nilikuheshimu kama mama jasiri sana. Historia ya maisha yako inaonesha umepitia mitihani mingi, kwa namna ambavyo umepambana na kuvuka viunzi hivyo, hakuna ambaye anaweza kuwa na shaka na wewe zaidi ya kukupongeza na kukuona ni mfano wa kuigwa.

Ulipambana sana kutetea uhai wa mumeo hadi pale Mungu alipomchukua. Nikwambie Watanzania walikupa heshima ya juu. Mimi mwenyewe nilikuheshimu sana. Sikuwahi kutarajia kama siku moja unaweza kushusha heshima yako kirahisi kama wafanyavyo baadhi ya wasanii.

Sikuwahi kuwaza kama kuna siku ninaweza kukuona umevaa mavazi ya ajabu kama wafanyavyo baadhi ya wenzako, achilia mbali ulevi wa kupindukia.

Niliamini wewe ndiye mtu wa kukemea wenzako wanaotoka nje ya mstari wa kujiheshimu.

Licha  ya kukuheshimu huko kwa muda mrefu, juzikati ulifanya tukio ambalo nilipoliona, akili yangu ilishindwa kuamini kama ni wewe yule ninayekuheshimu. Nazungumzia matusi mazito uliyoyaporomosha kwenye mtandao wa Instagram.

Ulimtukana mmoja wa mashabiki wako matusi mazito ya nguoni. Najua kabisa kwamba alikuudhi na kama binadamu unakasirika, lakini siku zote kabla ya kufanya jambo lolote lazima kwanza uangalie nafasi yako katika jamii.

Huwezi kumuona chizi anakutukana eti na wewe ukamtukana ili kumkomoa. Mwenye busara na hekima, akitukanwa na chizi, hukaa kimya na mwisho wa siku watu hubaini nani ni chizi!

Kwa matusi uliyomlipizia yule shabiki wako, waungwana walikujadili wewe uliyejibu badala ya shabiki wako.

Walikuona hukutumia busara. Kwa nafasi yako katika jamii, ukisema umjibu kila atakayekutukana, utawatukana wangapi? Jamii nayo itakuelewaje?

Nikuambie tu dada yangu hukufanya kitu kizuri hata kidogo, wewe ni staa mwenye heshima kubwa, huwezi kutukana matusi mazito kiasi kile hadharani, tena kwenye akaunti yako ambayo unaitumia kufanya biashara mbalimbali.

Binafsi tangu siku ile niliposoma posti yako nilijisikia vibaya, sikutegemea. Ningekushauri, ili kurejesha heshima yako, omba radhi na kubadilika. Kwa leo ni hayo tu.

Wasalaam

By GPL

KUNGURU: NIMETUMWA SANA POMBE NA WASANII BONGO MOVIE

IMELDA MTEMA
MSANII wa sinema za Kibongo, Brenda Malembeka ‘Kunguru’ ameibuka na kuanika ukweli wa maisha yake kuwa kabla ya kutoka kisanaa, aliteseka sana kwa kutumwa pombe na wasanii waliokuwa tayari na majina makubwa.
Msanii wa sinema za Kibongo, Brenda Malembeka ‘Kunguru’.
Akizungumza na mwanahabari wetu, Kunguru alisema kwa kipindi hicho ilimlazimu akubali kutumwa pombe na mastaa kwani lengo lake lilikuwa ni kupatiwa nafasi ya kucheza uhusika ukuu. “Nilikubali sana kutumwa pombe na mastaa wakubwa ili lengo langu litimie, nashukuru Mungu kwa sasa nimepata shavu kwenye filamu inaitwa Asante iliyoandaliwa na Masai Media Group,” alisema Kunguru.

Aunt Ezekiel Atoboa Kuhusu Wasanii wa Bongo Movies Kujitengenezea ‘Skendo’

Staa mrembo wa Bongo Movies, Aunt Ezekiel ‘Mama Kijacho’ amesema baadhi ya wasanii wa bongo movies hawajitambui ndio maana kazi zao nyingi hazina mvuto  badala yake nguvu nyingi wameelekeza kubuni skendo wakitarajia ndio zitawatoa kisanaa.

Alisema wasanii wengi wanatumia muda mwingi kutafakari jinsi ya kutengeneza skendo ili watume kwenye mitandao na kuandikwa kwenye magazeti lakini hawana ubunifu  wa kutengeneza filamu zenye ushawishi kwenye jamii.

Aunt ambae kwenye filamu ya Chozi la Wanjaa amecheza kama mke wa Dude alisema kwamba endapo wasanii wanaofanya mchezo huo hawata badilika ni ukweli usiopingika  kwamba soko la filamu  inchni litaendelea kudumaa kama ilivyo sasa.

Ni ukweli kwamba baadhi ya wasanii wa filamu hawajitambui kwani akili yao wameelekeza kwenye kutengeneza skendo badala ya kubuni namna ya kuigiza filamu ambazo zinaweza kuwa na mvuto kwenye jamiiinayoziangalia kinyume na hapo tutaendelea kusaka wachawi wanaoua soko letu’- Aunt Ezekiel alilieza gazeti la Filamu

Mdau una maoni gani juu ya hoja hii ya wasanii kutengeneza skendo, je ni kweli? Msanii gani unahisi ndio kazi yake.

ETHIDEI YA MTOTO WA DAVINA, NISHA ATIA AIBU BAADA YA KULEWA POMBE!

POMBE si chai! Msemo huu ulitimia hivi karibuni baada ya staa wa filamu za Kibongo, Salma Jabu ‘Nisha’ kuzidiwa na kilevi na kuanza kushindana kukata mauno na kusababisha azingirwe na wanaume waliovutiwa naye.
Staa wa filamu za Kibongo, Salma Jabu ‘Nisha’ akikata mauno.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Jumatano iliyopita katika sherehe ya bethidei ya mtoto wa msanii mwenzake, Halima Yahya ‘Davina’ iliyofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Lamada jijini Dar ambapo kulikuwa na vyakula na vinywaji vikali vya kila aina.
Nisha ambaye alikuwa amevalia kikaptula cha ‘jeans’ na kujistiri na mtandio, baada ya kukolea ulevi aliutupa mtandio na kuacha sehemu kubwa ya mwili wazi kisha  kukata mauno kushindana na mademu mcharuko waliokuwa ukumbini hapo kiasi cha kuwapagawisha wanaume wakware ambao walimvaa na kutaka kucheza naye.

Davina akiwa na mwanaye.
“Duh yaani Nisha leo ametia aibu, si kawaida yake nahisi mitungi imemzidi. Ameamua kujiachia kupitiliza, hebu mwangalie anavyokata mauno watoto wanamuangalia, aibu hii,” alisikika mualikwa mmoja akimwambia mwenzake.
Mauno mauno.
Hata hivyo, Davina alipoona baadhi ya waalikwa wanazidisha kusaula na kukatika, aliomba kipaza sauti na kuwataka wasifanye hivyo kwani sherehe ni ya mtoto.Sherehe hiyo ilihudhuriwa na mastaa kibao akiwemo Jeniffer Kyaka ‘Odama’, Mayasa  Mrisho ‘Maya’, Mike Sangu, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ na wengine wengi ambao  baadhi yao walionekana wakiwa wamekolea kilevi.

JB AFUNGUKIA KABURI LA KUAMBIANA...ASEMA SASA HAWEZI KULIJENGEA KWA KUA HANA HELA!

Staa wa filamu Bongo, Jacob Steven ‘JB’.
GLADNESS MALLYA
BAADA ya wadau mbalimbali kuhoji kwa nini staa wa filamu Bongo, Jacob Steven ‘JB’ ameliacha kaburi la aliyekuwa mwongozaji wa filamu katika kampuni yake, marehemu Adam Kuambiana mwenyewe amefunguka kwamba hali ya kifedha ni ngumu kwa sasa.
Akipiga stori na Centre Spread, JB alisema anatamani kulikarabati kaburi la Kuambiana ambalo limetoboka na mpango huo upo kwenye ratiba yake ila kwa sasa hali ya kifedha ni ngumu ikiwa nzuri ataanza ujenzi wake mara moja.
“Unajua ni muda mrefu nilikuwa safarini Mwanza, sasa nimerudi nitafanya mchakato hali ya kifedha ikiwa nzuri nitalijengea kaburi hilo maana nimekuwa nikiulizwa sana kuhusu hili lakini itambulike kwamba Kuambiana alikuwa ni kama mdogo wangu wa damu hivyo lazima nilijengee,” alisema JB.

IMEBAINIKA..!! MASTAA BONGO MUVI NJAA TUPU!

Waandishi wetu
Imevuja! Uchunguzi uliofanywa na Ijumaa Wikienda umebaini kwamba mastaa wengi wa sinema za Kibongo wapo katika hali ngumu kiuchumi kutokana na soko la filamu kudorora huku wizi wa kazi zao na kusitishwa mikataba yao na makampuni makubwa ya usambazaji vikichangia.
Uchunguzi huo umebaini kwamba moja ya makampuni yaliyositisha mikataba ya wasanii ni Steps Entertainment ambao wamesababisha mastaa kibao kushindwa kutengeneza muvi kwa kuwa awali walikuwa wakipewa bajeti na Steps kisha kuwauzia kwa bei ya mapatano.
Ilibainika kwamba baada ya Steps kuachana na utaratibu huo na kudai kuwa wanachukua muvi zilizoandaliwa na makampuni binafsi za mastaa wachache kama Jacob Steven ‘JB’, Athuman Amri ‘Mzee Majuto’, Vincent Kigosi ‘Ray’ na wengine wenye makampuni binafsi.
Mmoja wa mastaa wakubwa wa filamu, Musa Issa ‘Cloud 112’ alikiri kuwepo kwa hali hiyo huku akifafanua kuwa Steps kuna wakati inakuwa kwenye kipindi kigumu.

WAMEONDOKA NA BONGO MUVI YAO!

Marehemu Steven Charles Kanumba enzi za uahi wake.
Kwenye familia yangu mama alipotangulia mbele ya haki, familia ilikuwa juu mno kwa kila kitu lakini ghafla iliyumba vibaya hivyo tukapata kazi ya kuisimamisha upya, jambo ambalo limekuwa gumu kufikia pale tulipokuwa awali. Ishu hapa ni mchango wa mtu katika eneo lake. Anapoondoka ni lazima ‘gepu’ lake huonekana na kuliziba inahitaji nguvu kubwa na ya ziada.
Kanumba
Aprili 7, mwaka huu ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya miaka mitatu tangu alipofariki dunia nguli wa sinema za Kibongo, marehemu Steven Charles Kanumba.
Ni katika kipindi ambacho mastaa wa tasnia hiyo wamekuwa wakiangua vilio kwamba sinema za nyumbani kwa sasa haziuzi. Kwa kifupi hazilipi!
Wapo waliokiri waziwazi kuwa kuondoka kwa staa huyo kumeliangusha soko hilo kwa kuwa ushindani aliouonesha na mwigizaji mwenzake, Vincent Kigosi ‘Ray’ haupo tena. Na wengine nao wamekosa ile chachu ya moyo wa ushindani. Matokeo yake wamebaki palepale siku zote na wengine kunyamaza kabisa. Hawasikiki!
Marehemu Adam Kuambiana enzi za uhai wake.
Ukweli ni kwamba mastaa wengi wa tasnia hiyo kwa sasa wanaishi maisha magumu ya kuungaunga. Wana majina makubwa lakini hawana kodi za nyumba. Wamebaki na magari yaleyale ambayo sasa yanawatoa jasho kujaza mafuta na kuyafanyia matengenezo. Yamekuwa mikweche. Wamebaki kuombaomba.
Mastaa mbalimbali wamekiri hili:
JB
Jacob Steven ‘JB’ ni mmoja wa waigizaji wakubwa Bongo ambao wanauza zaidi hasa anapokuwa na mchekeshaji Amri Athuman ‘Mzee Majuto’.Kwa mujibu wa JB tasnia ya filamu inaangukia katika kifo kutokana na kwamba kwa sasa haziuzi na uwepo wa maharamia.JB anasema kuwa hali hiyo inawafanya wasambazaji kuanza kuikimbia tasnia hiyo na wengine kushusha bei ya filamu.
Dude
Kauli ya JB inaungwa mkono na mwigizaji mwingine mkubwa, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ambaye anaamini kuwa kuna kitu cha kufanya ikiwemo watu kuwekeza kwenye tasnia hiyo. Pia kuna suala la elimu kwa waigizaji, madairekta, maprodyuza na wasambazaji wazawa kisha serikali itenge bajeti kama ilivyo kwa Nollywood (Nigeria) na Hollywood (Marekani) kwa kuwa ni tasnia inayoajiri watu wengi.
Dk. Cheni
Mara kadhaa, mwigizaji Mausen Awadh ‘Dk. Cheni’ amekuwa akionesha wasiwasi wake juu ya kudorora kwa tasnia hiyo. Wapo baadhi ya waigizaji ambao hawakubali ukweli lakini Dk. Cheni ni miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa waliokiri kwamba kifo cha Kanumba kiliathiri kwa kiasi kikubwa tasnia ya sinema Bongo.Mbali na Kanumba, pia wapo maprodyuza na madairekta waliotangulia mbele ya haki.
Adam Kuambiana
Ukizungumza na mastaa wengi wa tasnia hiyo, hakuna anayebisha kuwa marehemu Adam Kuambiana (alifariki dunia Mei 17, mwaka jana) alikuwa kichwa kwenye tasnia hiyo. Alifanya kazi na kampuni nyingi za kutengeneza sinema Bongo ikiwemo Jerusalem Films Productions chini ya JB. Kifo cha jamaa huyo kimeacha pengo kubwa.
Marehemu George Otieno ‘Tyson’ enzi za uhai wake.
Tyson
Pia kifo cha George Otieno ‘Tyson’ aliyekuwa dairekta bora kabisa Bongo aliyefariki dunia Mei 30, mwaka jana, nacho kinatajwa kufifisha tasnia hiyo.Mbali na sinema za nyumbani, Tyson alifanya kazi kubwa kwenye michezo ya kuigiza ya runingani iliyosaidia kukuza tasnia hiyo Bongo.
Tatizo hili hawalioni!
Mbali na kuondoka kwa madairekta hao ambao kinachoonekana wengi wanaamini kuwa wameondoka na tasnia yao, lipo tatizo ambalo wengi hawalioni.Kwa sasa sehemu kubwa ya jamii yetu hainunui sinema za nyumbani kwa sababu wana chansi ya kuziona bure kupitia ving’amuzi.
Nini cha kufanya?
Kama walivyosema baadhi ya waigizaji kwenye makala haya, haina ubishi kwamba tasnia hiyo inaajiri vichwa vingi hivyo lazima jitihada zifanyike za kuinusuru.Ni vizuri waigizaji wakarejesha ule umoja wa Kaole Sanaa Group.Ni wakati muafaka wa kuweka pembeni majungu, visasi, bifu za kipuuzi, unafiki na wengine kujiona miungu watu kwani anguko tunalolishuhudia halibagui. Tunajenga nyumba moja, ya nini kugombea fito?

ROSE NDAUKA ASEMA BAADA YA KANUMBA KUFARIKI BONGO MOVIE HAKUNA USHINDANI TENA

Kama wewe ni Mmoja wa Wapenzi wa Filamu za Nchini Tanzania na unafuatilia Vizuri basi utakubaliana na Rose Ndauka Kwamba Baada ya Kufariki STEVEN KANUMBA
Rose Ndauka Ameongea na @DjHaazu na kusema Steven Kanumba aliipigania sana Tasnia ya Filamu Nchini Tanzania Haswa kwa jitihada zake kukuza Wasanii wenzake ambapo kwa Moyo wake kwa kushirikiana na Wasanii wenzake Waliifikisha Sanaa ya Filamu Tanzania Hapo ilipo ila hadi sasa Hakuna Hatu Nyingine ambayo Wasanii wa Filamu Tanzania Wamepiga Zaidi ni Kuporomoka kwa Kiwanda cha Bongo Movie TZ.
Hta hivyo Rose ambaye yuko kwenye Tasnia ya Filamu Nchini Tanzania kuanzia Mwaka 2007 Amesema Wao Kama Wasanii kwa sasa wanatakiwa kushikamana na kufanya Mabadiliko ili Kuendeleza Kile alichokuwa anakifanya ambacho ilikuwa Kuhakikisha Sanaa ya Tanzania Inajulikana Kimataifa Zaidi.
Cha mwisho amewataka Watanzania na Wadau wao Kuendelea Kuwashika Mkono kwa kuwapa Support Japo pia ainawezekana kuna Wakati wamewadissapoint.

RAY AMSALITI CHUCHU KWA HUSNA, WANASWA USIKU

MUIGIZAJI nyota wa filamu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’, amedaiwa kumsaliti mpenzi wake wa siku nyingi, Chuchu Hans baada ya kukutwa akiwa amepozi kimahaba na mshiriki wa Miss Tanzania mwaka 2011, Husna Maulid katika Ukumbi wa Escape One, Mikocheni jijini Dar, hivi karibuni.Muigizaji nyota wa filamu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ akipozi kimahaba na Husna Maulid.
Wawili hao waliokuwa wamepakatana, walikutwa katika ukumbi huo wakati bendi mbili kubwa za muziki wa dansi nchini, FM Academia na The African Stars ‘Twanga Pepeta’ zilipokuwa zikiangusha burudani kabambe ya kushindana.
Uwepo wa Ray na Husna ulitafsiriwa kuwa ni usaliti kwani muda wote waliokuwa ndani ya ukumbi huo wawili hao walikuwa wamegandana kimahaba huku wataalamu wa ubuyu wakikazia madai kwa kusema wawili hao ni wapenzi.
Husna Maulid akisisitiza jambo kwa Ray.
“Sasa wewe kusoma hujui hata picha huoni? Hawa watakuwa ni wapenzi tu, haiwezekani mtu mpakatane, mpeane kampani kiasi hiki na mtu ambaye siyo mtu wako,” alisikika shuhuda mmoja.
Ray ambaye kabla ya kuwa na Chuchu aliwahi kutoka kimapenzi na mwigizaji Blandina Changula ‘Johari’ na Ruth Suka ‘Mainda’, alionekana kufurahia kumpakata Husna huku wakipeana kampani ya kuzungumza, lakini alipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kugundua kuwa alikuwa akifuatiliwa na kamera ya paparazi wetu.
Kutokana na mazingira ya wawili hao ukumbini hapo, paparazi wetu alishindwa kuzungumza nao juu ya ishu hiyo na hata alipowatafuta kwa simu siku iliyofuata, simu zao ziliita bila kupokelewa (huenda walijua wataulizwa nini).Lakini Chuchu, ambaye ndiye ‘mmiliki’ wa Ray hivi sasa, alipoulizwa kama anajua lolote juu ya ukaribu wa watu hao, alishtuka na kudai haamini kama Ray anaweza kumsaliti au amewahi kupiga picha na Husna za kimahaba.
Muigizaji nyota wa filamu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray.
“Khaa! Unasemaje? Mimi siamini labda kama kuna picha zao za pamoja naomba unitumie Whatsapp nizione maana nashindwa niongee nini, sikujua kama walienda popote Ray na Husna.”
Mwanahabari wetu alimtumia picha hizo Chuchu lakini hadi tunakwenda mitamboni, mrembo huyo hakuwa amejibu kitu chochote.

CHUCHU AZIRAI NDANI YA JENEZA! NUSU AFE WAKATI ANAIGIZA



HII ni kali ya mwaka! Staa wa sinema za Bongo, Chuchu Hans amejikuta akizirai ndani ya jeneza wakati akiigiza sini ya kifo kwenye filamu, Amani limeinyaka.
 
Staa wa sinema za Bongo, Chuchu Hans akiwa kwenye jeneza.
Chuchu alikumbwa na hali hiyo hivi karibuni akiwa ‘lokesheni’ ya kuigizia filamu hiyo maeneo ya Mbezi ya Kimara jijini Dar es Salaam ambapo sanjari na yeye, msanii mwingine aliyecheza nafasi ya mwanakwaya naye alipoteza fahamu wakati kipande hicho kikirekodiwa.
TATIZO UHALISIA, WASIWASI
Chanzo kimoja kutoka ndani ya kundi la wasanii waliokuwa wakiigiza filamu kinasema kuwa, Chuchu alikumbwa na hali hiyo kutokana na wasiwasi na ujasiri wa kuuvaa uhusika.

“Awali, Chuchu alionesha wasiwasi wa kuigiza kipande hicho cha kumwonesha yeye yumo ndani ya jeneza akiwa amefariki dunia kwa ugonjwa kama wa kichaa kilichotokana na msongo wa mawazo baada ya kubakwa.
“Mbaya zaidi, mwongozaji naye alisema ni lazima akiwa amelala ndani ya jeneza awekewe pamba za kuziba matundu ya pua kama maiti wanavyowekewa,” kilisema chanzo.
...Waombolezaji wakilia kwa uchungu.
ILIKUWA WAKATI AKIAGWA
Chanzo kikazidi kudai kwamba, taharuki yote hiyo ilitokea pale, ‘mwili’ wa Chuchu ukiagwa kwenye Kanisa la Sabato, Mbezi, Dar ambapo waombolezaji walipokuwa wakipita, binti yake, Farha (9) aliangua kilio kilichomfanya Chuchu ajikute akikata pumzi ghafla!

AMALIZA SINI, ASHINDWA KUAMKA
Ikaelezwa kwamba, ilikuwa wakati kipande hicho kimeisha huku binti yake akiendelea kulia kwa kumwona mama yake ndani ya jeneza, Chuchu hakuamka ili kuendelea na vipande vingine hali iliyowafanya watu wazima kumkagua na kugundua alizirai.

“Watu walianza kupagawa, wengine walijua ameshapoteza maisha. Lakini Mungu mkubwa Chuchu akazinduka na kumkuta mwanaye bado akilia kwa nguvu. Ilibidi wasanii wengine waingilie kati kumtuliza,” kilisema chanzo.

Waombolezaji wakiwa na simanzi.
MWINGINE AITIWA MCHUNGAJI
Wakati Chuchu ‘akifufuka’, yule msanii aliyeigiza nafasi ya mwanakwaya yeye alikuwa bado chini amelala chali akiwa hajitambui kwa kile kilichokuwa kikiendelea.“Yule mwenzake ilibidi aitwe mchungaji wa kanisa hilo ambaye alikuwa jirani kwa ajili ya kumwombea japo mchungaji wa filamu hiyo alikuwa ni msanii Jimy Mafufu,” kilisema chanzo.

MASWALI ENEO LA TUKIO
Baadhi ya wasanii walianza kujiuliza nini kilisababisha hali ile kwani ilionekana kama kuna roho chafu aliyetaka kufanya mauaji ya makusudi.

“Wengine waliuliza kama kuna mtu ana vitu kama hirizi au chanjo ya mambo ya kishirikina, ikaonekana hakuna. Lakini maswali yalikuwa mengi sana,” kilisema chanzo.

Jeneza likiandaliwa kwa ajili ya mazishi.
CHUCHU AONGEA NA AMANI
Baada ya kuinasa taarifa hiyo, Amani lilimsaka Chuchu kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumuuliza ambapo alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Huyu hapa:  “Yaani siwezi kueleza juu ya ile filamu maana ilikuwa ni hatari tupu na sijui hata mama yangu akiiona itakuaje kwa kweli.
“Lakini kwenye ile sini yangu ndiyo ilikuwa ikihitaji hivyo, nilale kama maiti kweli na huwezi amini lilichimbwa hadi kaburi la ukweli. Mimi nilizimia si chini ya  mara moja. Pumzi yangu ilikata hasa nilipomsikia mwanangu akilia.”
 
CHUCHU ANAWEZA ASIWE SAWA KISAIKOLOJIA
Kwa mujibu wa maswali ya kisaikolojia kwa wasanii wa maigizo, baada ya msanii kuigiza filamu inayohusu ukatili wowote, kumwaga damu, mapenzi ya kupitiliza, kifo au jambo lolote ambalo ni chungu kwa ubinadamu ni lazima aombewe na viongozi wa dini ili kuifukuza roho hiyo ya kuigizia.

Wanasaikolojia wanasema kuwa, msanii akiigiza nafasi kama hizo na kujiacha hivihihivi kuna hatari baada ya muda kuambukizwa na uigizaji huo ikawa ndiyo maisha yake ya kila siku. Ndiyo maana baadhi ya wasanii wa filamu duniani kote wanaishi maisha ya sawasawa na wanavyocheza filamu.      

‘UKAWA’ YAZALIWA BONGO MOVIE LIKIONGOZWA NA STEVE NYERERE!

WASANII wa filamu ambao hivi karibuni waliripotiwa kujitoa katika kundi la Bongo Movie Unity wamedaiwa kuunda la kwao linalojulikana kama Ukawa ambalo litakuwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti aliyetimuliwa, Steven Mengere maarufu kama Steve Nyerere.
Baadhi ya Wasanii wa bongo Movies waliokuwa pamoja katika uongozi kabla ya mzozano.
Baadhi ya wasanii wanaotajwa kuunda kundi hilo kwa mujibu wa chanzo chetu makini ni pamoja na Devotha Mbaga, Salama Salmin ‘Sandra’, Halima Yahya ‘Davina’ na wengineo.
“Yaani sasa hivi haya makundi mawili kuna vita kali sana, kila moja linataka lionekane kwamba lina nguvu kuliko lingine, hata jina la Bongo Movie Unity limebadilishwa sasa hivi linaitwa Bongo Movie Stars,”kilisema chanzo hicho.Aliyekuwa Katibu msaidizi wa Bongo Movies Unity, Devotha Mbaga.
Mussa Issa ‘Cloud’ alikiri kubadilishwa jina kwa Bongo Movie Unity na pia amesikia habari za kuwepo kwa kundi la Ukawa wakati Steve Nyerere alisisitiza kuwa bado ni mwanachama wa Bongo Movie Unity na kwamba mtu anayetaka kuwagombanisha wasanii anajulikana.

AISHA BUI AZUA TIMBWILI, NI KATIKA KUDAI KULIPWA FEDHA ZA FILAMU!

Pamechimbika! Staa wa sinema za Kibongo, Aisha Bui amezua timbwili la kufa mtu katika ofisi za kusambaza filamu za Yuneda zilizopo Mbagala jijini Dar baada ya wasambazi hao kushindwa kumlipa kwa wakati.
Staa wa sinema za Kibongo, Aisha Bui akiwaka kwa mmoja wa wahusika wa ofisi za kusambaza filamu za Yuneda, Mbagala.
Mtiti huo ulioshuhudiwa na wanahabari wetu ulijiri wikiendi iliyopita, maeneo hayo ya Mbagala ambapo Aisha aliongozana na shemeji yake katika ofisi hizo na kuibua tafrani kubwa iliyokusanya kadamnasi na kufunga mtaa kwa muda.
Aisha Bui mara baada ya kuvunja kioo cha mlango.
Kwa mujibu wa Aisha, amekuwa akitimba kwenye ofisi hizo mara kwa mara akiomba alipwe chake lakini amekuwa akipigwa kalenda tangu Aprili, mwaka huu. Aisha alilifungukia Ijumaa Wikienda kwamba, kuna siku mkurugenzi wa kampuni hiyo aitwaye Ngeze alimwita ofisini kwake ili kumlipa lakini alipofika alimpa kiasi cha shilingi milioni mbili na nusu, jambo ambalo lilikuwa kinyume na makubaliano.
Aisha Bui akiwa na jiwe lililotumika kuvunjia mlango wa kioo wa ofisi hizo.
“Filamu yenyewe nimeigiza kabla sijajifungua hadi mtoto wangu sasa ana miezi sita. Kama mtu ndiyo unategemea fedha za filamu yako ndiyo uendeshee maisha, halafu mtu halipi, sasa utaishije?
 Staa huyo alisema alikuwa akimpigia simu mara kwa mara mwisho mkurugenzi huyo aliamua ‘kum-block’ kwenye simu hivyo akawa amekosa mawasiliano naye.
Wananchi wakishuhudia varangati lililoanzishwa na Aisha Bui. 
Aisha alipofika ofisini hapo alishikwa na ghadhabu baada mhasibu wa kampuni hiyo kumwambia hakuwa na namba ya bosi wake wakati alijua akifika tu angepewa fedha hizo hivyo akashikana naye mashati na kuanza kuzipiga ambapo Aisha alisukumwa akadondoka pwaa!
Kitendo cha kusukumwa, kilimpandisha hasira Aisha na kuamua kuchukua jiwe ambalo lilishindwa kufungua mlango hivyo alichukua nondo na kuvunja mlango huo ambapo wafanyakazi walijifungia kwa ndani ili kumzuia asiingie ndani.
Aisha Bui akiondoka eneo la tukio.
Wanahabari wetu walipomfuata  Ngeze kujua kulikoni kumtia mbaroni Aisha alisema alivamiwa na staa huyo na mabaunsa ambao walivunja ofisi pamoja na kushukua ‘laptop’ na fedha.
Hadi gazeti hili linaondoka eneo hilo, Aisha na shemeji yake walikuwa bado wameshikiliwa na Polisi wa Kituo cha Maturubai, Mbagala.

FILAMU YA MAPENZI YA MUNGU KUINGIA SOKONI WIKI HII

Mwezi, Wiki na Sasa siku zimebaki kwa ile Filamu Mpya na ya Kusisimua ya MAPENZI YA MUNGU Kuingia Sokoni ambayo imewakutanisha wasanii mahiri wa hapa hapa Tanzania ambapo Mmoja kati ya Wasanii waliocheza filamu hiyo Ni Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya anayejulikana kama Linah Sanga, kwa Kushirikiana na Elizabeth Michael bila Kumsahau Flora Mtegoha ambae ni Mama Mzazi wa Marehemu Steven Kanumba watakuwa ndani ya filamu Mpya iitwayo MAPENZI YA MUNGU...Ni Filamu ambayo Kisa chake na Mafunzo yake yanasisimua lakini Pia ni Moja kati ya filamu ambayo kiukweli ina hadhi na vigezo vya kimataifa......
Nimefika hapa leo sio kwa Ujanja wangu Bali ni Kwa "Mapenzi ya Mungu..."
Filamu ya "Mapenzi ya Mungu" ni moja ya filamu ambayo Msanii Linah pamoja na Mama Mzazi wa Marehemu Kanumba wameonyesha uwezo wa hali ya juu na kuthibitisha kuwa kweli Sanaa ni Kazi.
Filamu ya "Mapenzi ya Mungu" itakuwa Sokoni Kuanzi Wiki hii Kwa Wauzaji wa Filamu kote Nchini.
Filamu hii itasambazwa na Kampuni mahiri ya Proin Promotions Ltd.
Older Posts
© Copyright ZEE LA UDAKU | Designed By Code Nirvana
Back To Top